1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sharon aagwa rasmi

13 Januari 2014

Wananchi wa Israel Jumatatu(13.01.2014)wametowa heshima zao za mwisho kwa Waziri Mkuu wa zamani Ariel Sharon mtu ambaye amesifiwa kuwa ni shujaa wa vita nchini mwake na kuonekana kuwa mhalifu wa vita na nchi za Kiarabu.

Maafisa wa jeshi la Israel wakiwa na jeneza la Ariel Sharon katika bunge la Israel Knesset mjini Jerusalem. (13.01.2014).
Maafisa wa jeshi la Israel wakiwa na jeneza la Ariel Sharon katika bunge la Israel Knesset mjini Jerusalem. (13.01.2014).Picha: Reuters

Wananchi wa Israel leo wametowa heshima zao za mwisho kwa Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Ariel Sharon katika ibada mbili za mazishi kwa mtu ambaye amesifiwa kuwa ni shujaa wa vita nchini mwake na kuonekana kuwa ni mhalifu wa vita kwa ulimwengu wa Kiarabu.

Makamo wa Rais wa Marekani John Biden na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steimeir ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria ibada ya mazishi mbele ya bunge la Israel wakati jeneza la Sharon lililofunikwa bendera ya Israel likiwa limewekwa uwanjani.

Akiwasilisha rambi rambi zake Biden amesema Sharon alikuwa ni mtu ambaye nyota iliokuwa ikimuongoza ilikuwa ni usalama na uhai wa taifa la Israel.

Biden amesema kwa ushujaa mkubwa Sharon katu,katu,katu hakuyumba kwenye lengo hilo.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akisalimiana na Makamo wa Rais wa Marekani John Biden wakati wa ibada ya mazishi ya Sharon.(13.01.2014).Picha: Reuters

Rais Shimon Perez wa Israel naye amesema leo wanamsindikiza kwenye mapumziko yake ya milele mwanajeshi,mwanajeshi wa aina yake,kamanda ambaye alikuwa akijuwa namna ya kupata ushindi.

Sharon alifariki akiwa na umri wa miaka 85 hapo Jumamosi baada ya kupoteza fahamu kwa miaka minane kulikosababishwa na kiharusi.

Kifo chaibuwa mjadala

Kifo chake kimeanzisha upya mdahalo juu ya haiba yake wakati maadui zake wakilaani utendaji wake wa kikatili wakati wa operesheni za kijeshi huku marafiki zake wakimpongeza kuwa gwiji wa mikakati ambaye aliishtua dunia hapo mwaka 2005 kwa kuwaondowa majeshi na walowezi wa Kiyahudi kutoka Ukanda wa Gaza ambayo ni ardhi ya Wapalestina.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema ingawa hakuwa anakubaliana kwa kila kitu na Sharon katika masuala ya sera hususan suala la kujiondowa Gaza amepongeza kujitolea kwa kiongozi huyo wa zamani kwa usalama wa Israel.

Amesema "Wananchi wa Israel watamuenzi Ariel Sharon moyoni mwao milele kama mmojawapo wa viongozi wao na makamanda muhimu."

Rais Shimon Peres wa Israel na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu wakisalimiana na jamaa wa familia ya Sharon wakati wa ibada ya mazishi. (13.01.2014).Picha: Reuters

Sharon aliongoza mashambulizi ya kijeshi katika vita kadhaa na nchi za Kiarabu,alitanuwa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi yaliojengwa kwenye ardhi ambayo Wapalestina walikuwa wanatake iwe taifa lao na wakati alipokuwa waziri mkuu ndio alipopitisha uamuzi wake huo wa kushtua wa kujitowa Gaza hapo mwaka 2005.

Kisa cha kuchukiwa na Waarabu

Sharon alikuwa akichukiwa sana na Waarabu kwa kile walichokuwa wakikiona kuwa sera zake kali na za uchokozi ikiwa ni pamoja na uvamizi wa Lebanon hapo mwaka 1982 katika harakati za kujaribu kuwatimuwa Wapalestina nchini humo pamoja na kutumia nguvu za kijeshi kuwaondowa kwa nguvu walowezi wa Kiyahudi katika makaazi yao katika ardhi ya Wapalestina waliokuwa wakiikalia kwa mabavu.

Jeneza la Ariel Sharon likiwa nje ya bunge la Israel mjini Jerusalem.(13.01.2014)Picha: Reuters

Alilazimika kujiuzulu kama waziri wa ulinzi hapo mwaka 1983 baada ya uchunguzi wa Israel kusema kuwa alikuwa anawajibika binafsi kwa kushindwa kuzuwiya mauaji makubwa ya mamia raia wa Kipalestina katika makambi ya wakimbizi nchini Lebanon ya Sabra na Shatila yaliofanywa na washirika wa Israel wanamgambo wa Kikristo nchini Lebanon.

Sharon anazikwa mchana huu kwenye shamba lake lilioko kwenye jangwa la Negev pembezoni mwa kaburi la mke wake Lily.

Mwandishi: Mohamed Dahman, Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman