Shehbaz Sharif achaguliwa kwa muhula wa pili Pakistan
3 Machi 2024Spika wa bunge Ayaz Sadiq ametangaza kwamba Sharif alipata kura 201 na kumshinda Omar Ayub aliyepata kura 92 katika Bunge la Kitaifa lenye wanachama 336.
Washirika wa waziri mkuu wa zamani Imran Khan walipiga kelele bungeni kupinga uteuzi huo, kwa madai ya wizi wa kura mwezi uliopita.
Soma pia: Vyama vya kisiasa Pakistan vyaunda serikali ya muungano
Uchaguzi wa Februari 8 ulighubikwa na ukosoaji kutokana na kuzimwa kwa mtandao wa simu, kamatakamata na vurugu pamoja na kucheleshwa kwa matokeo.
Baada ya kuapishwa,Shehbaz Sharif atahitaji kwa mara nyingine tena kuomba mkopo kutoka kwa Shirika la Fedha la Ulimwenguni IMF huku muda wa mkataba wa mkopo wa sasa ukitarajiwa kumalizika mwezi ujao.
Pakistan inaendelea kughubikwa na mzozo wa kiuchumi huku mfumuko wa bei ukisalia kuwa juu, karibu kwa asilimia 30, na wakati huo huo ukuaji wa uchumi wa nchi hiyo umepungua na kufikia karibu asilimia 2.