1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMexico

Sheinbaum awa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa rais wa Mexico

3 Juni 2024

Claudia Sheinbaum ameingia kwenye historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa kuwa rais nchini Mexico katika ushindi wa kishindo jana Jumapili.

Rais mpya wa Mexico Claudia Sheinbaum
Mgombea urais wa chama tawala Claudia Sheinbaum akihutubia wafuasi baada ya kukamilika kwa zoezi la kupiga kuraPicha: Fernando Llano/AP Photo/picture alliance

Tume ya uchaguzi nchini humo INE imesema matokeo ya awali yameonyesha kuwa meya huyo wa zamani wa Mexico City ameshinda kwa kupata kati ya asilimia 58 na 60 ya kura katika uchaguzi wa jana Jumapili. 

Mamia ya watu waliokuwa wamebeba bendera wamemiminika barabarani huku wakiimba nyimbo na kucheza katika uwanja mkuu mjini Mexico City kusherehekea ushindi wa Claudia Sheinbaum.

Sheinbaum aliyeonekana mwenye bashasha, aliwashukuru wananchi wa Mexico, waume kwa wake waliojitokeza kumpigia kura.

Soma pia: Wamexico wapiga kura katika katika uchaguzi wa kihistoria

Katika hotuba yake ya ushindi, meya huyo wa zamani mwenye umri wa miaka 61 ameapa kuwa kamwe hatowaangusha wananchi wa Mexico.

"Naahidi kuiongoza Mexico katika njia ya amani, usalama, demokrasia, uhuru, usawa na haki.”

Amempongeza pia mpinzani wake mkuu Xochitl Galvez aliyekubali kushindwa.

Kiongozi huyo ambaye kitaaluma ni mwanasayansi, alijikingia kati ya asilimia 58 na 60 ya kura, kwa mujibu wa matokeo rasmi ya awali yaliotolewa na tume ya uchaguzi nchini humo.

Tume hiyo imeeleza kuwa, takriban asilimia 60 ya wapiga kura ndio waliojitokeza kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.

Wananchi wakiwa na bango lililosomeka 'Rais Claudia Sheinbaum' baada ya chama tawala nchini Mexico Morena kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa uraisPicha: Mahe Elipe/REUTERS

Idadi hiyo ilikuwa zaidi ya asilimia 30 mbele ya mpinzani wake mkuu, mfanyibiashara Xóchitl Gálvez na asilimia 50 mbele ya mwanamume pekee katika kinyang'anyiro hicho Jorge Alvarez Maynez.

Bi. Sheinbaum sasa atachukua nafasi ya rais anayemaliza muda wake Andres Manuel Lopez Obrador, mnamo Oktoba mosi.

Ameahidi kufuata nyayo na kuendeleza mikakati ya Lopez Obrador. Hata hivyo, ameweka wazi kuwa Obrador hatakuwa na ushawishi wowote katika serikali yake.

Wapiga kura walimiminika katika vituo vya kupigia kura katika taifa hilo la Amerika ya Kaskazini licha ya vurugu na ghasia kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo yanayotawaliwa na magenge ya wahalifu na walanguzi wa dawa za kulevya.

Uchaguzi huo ambao ulitajwa kuwa kati ya farasi wawili, Sheinbaum na Galvez, ambao wote ni wanawake, umetafsiriwa kama fursa adimu ya mabadiliko kwa wanawake nchini Mexico.

Wanawake wengi walipata hamasa ya kumpigia mwenzao kura ili kukata mizizi ya muda mrefu ya ulingo wa siasa kutawaliwa na wanaume katika nchi ambayo karibu wanawake au wasichana 10 wanauawa kila siku.

Soma pia: Biden, Trump kufanya ziara kinzani mpaka wa Marekani-Mexico

Takriban watu milioni 100 wamejiandikisha kama wapiga kura katika taifa hilo lenye idadi kubwa ya watu wanaozungumza lugha ya Kihispania.

Kando na rais mpya, wapiga kura pia waliwachagua wabunge na magavana katika majimbo manane pamoja na maelfu ya viongozi wa mitaa.

Licha ya wagombea wakuu wa urais kuwa wanawake, kampeni kuelekea uchaguzi huo ziligubikwa na ghasia na mashambulizi yaliyolenga wanasiasa.

Takwimu za serikali zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 20 waliuawa japo vyanzo vyengine vinasema idadi ya watu waliouawa katika vurugu kuelekea uchaguzi huo ni watu 37.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW