1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za kukabidhiwa wageni uraia wa Ujerumani

Oumilkher Hamidou12 Mei 2009

Kansela Angela Merkel amewakabidhi wageni 16 vyeti vya uraia

Kansela Angela MerkelPicha: AP


Kwa mara ya kwanza katika historia ya shirikisho la jamhuri ya Ujerumani,sherehe za kukabidhiwa wahamiaji hati za uraia wa Ujerumani,zimefanyika katika ofisi ya kansela mjini Berlin.

Katika sherehe hizo maalum zilizofanyika leo mjini Berlin,kansela Angela Merkel wa kutoka chama cha Christian Democratic Union-CDU,amewakabidhi wageni 16 vyeti vya uraia wa kijerumani.Kansela Merkel amewahimiza raia hao wepya wasijiweke kando."Mnaweza kuiamini nchini hii."Kansela Angela Merkel amesisitiza serikali ya muungano wa vyama vikuu inatoa kipa umbele kwa sera za kuwapatia wahamiaji uraia na kuwajumuisha katika maisha ya kawaida ya jamii humu nchini.

Kansela Merkel amesema

"Tunafurahi kuona mmeamua kuchukua uraia wa Ujerumani.Tunataraji mtachangia kuwapa moyo wengine pia kwasababu tunapendelea kuwaona wengi zaidi wakiamua kuchukua uraia wa Ujerumani.Tunatambua jukumu letu,tunajua kila wakati ambapo juhudi za kuwajumuisha wageni katika maisha ya jamii zinapoeleweka vyema na watu kupata moyo wa kuchukua uraia nchi yetu inakua inafaidika."

Mmojawapo wa raia hao 16 wepya,Dr. RAGHAVA REDDY KETHIRI ni mzaliwa wa India anaeishi Ujerumani tangu miaka 12 iliyopita.Yeye anasema:

""Kwakua nimekua nikiishi tangu miaka 12 iliyopita nchini Ujerumani,nnahisi ni jambo la maana kujiambatanisha vyema na maisha ya humu nchini.Na hiyo ndio sababu ya kupitisha uamuzi huu."

Upande wa upinzani Bündnis '90/ die Grüne na ule wa mrengo wa shoto,Die Linke unakosoa juhudi za serikali kuu za kuwapatia wageni uraia.Msemaji wa kundi la Die Linke linaloshughulikia masuala ya uhamiaji katika bunge la shirikisho,Sevim Dagdelen anasema tunamnukuu:" Anaepata uraia wa Ujerumani anastahiki pia kuvikwa nishani."Amezungumzia vizingiti wanavyokabliana navyo wageni wanaoomba uraia wa Ujerumani.Bibi Sevim Dagdelen anasema vizingiti hivyo ndio sababu inayowafanya wengi wa wahamiaji wa humu nchini wasiombe uraia wa Ujerumani.

Mwenyekiti wa chama cha Bündnis 90/Die Grüne,Cem ÖZDEMIR anasema ili "kuwapa moyo wahamiaji wawe wenyeji,kuna haja ya kuondolewa vizingiti vilivyoko na hasa linapohusika suala la uraia wa nchi mbili.

Wengi kati ya wenye kuomba uraia wa Ujerumani wanalazimika kuthibitisha wamerejesha uraia wao wa asili kabla ya kukubaliwa uraia wa Ujerumani.

Takwimu zinaonyesha katika kipindi cha mwaka jana idadi ya waliomba uraia wa Ujerumani ilifikia chini ya watu laki moja,idadi ndogo kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu sheria za kuomba uraia zilipofanyiwa marekebisho mnamo mwaka 2000.

Sherehe hizo zimefanyika katika wakati ambapo Ujerumani inaadhimisha miaka 60 tangu kuundwa kwake.


Mwandishi:Oummilkheir Hamidou/DPA

Mhariri:M.Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW