1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sherehe za miaka 30 ya Muungano wa Ujerumani

Oumilkheir Hamidou
3 Oktoba 2019

Wajerumani wanaadhimisha miaka 30 ya muungano. Sherehe za mwaka huu zinafanyika katika mji mkuu wa jimbo la Schleswig Holstein-Kiel. Kauli mbiu ya sherehe za mwaka huu inasema "Moyo wa ujasiri watuunganisha."

Tag der Deutschen Einheit 2019 | Jubiläum | Merkel in Kiel
Picha: picture-alliance/dpa/C. Rehder

Zaidi ya watu laki tano wanahudhuria sherehe rasmi za mwaka huu zinazofanyika katika mji mkuu wa jimbo la kaskazini la Schleswig-Holstein-Kiel. Rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier na Kansela Angela Merkel ni miongoni mwa wageni wa hishima wanaohudhuria sherehe hizo. Katika kuadhimisha siku ya muungano, Steinmeier aliwatunukia "tuzo ya wastahiki"-tuzo yenye hishma kubwa ya Ujerumani-Bundesverdienstkreuz, watu 25 wakiwemo pia wawakilishi wa vuguvugu la upinzani katika ile iliyokuwa ikijulikana zamani kama jamhuri ya kidemkorasi ya Ujerumani GDR sawa na wanaharakati wa mapinduzi ya amani. "Moyo wenu wa ujasiri umevunja ukuta" amesema rais wa shirikisho katika hotuba yake.

Sherehe za Siku ya Muungano mjini KielPicha: picture-alliance/dpa/C. Rehder

Onyo dhidi ya kuzuka tena ufa kati ya Mashariki na Magharibi

Katika misa iliyofanyika asubuhi katika kanisa la Mtakatifu Nikolai mjini Kiel wawakilishi wa makanisa ya Kikristo wamesifu mbele ya wawakilishi wa ngazi ya juu wa kisiasa, utamaduni na jamii, muungano wa Ujerumani uliopatikanma kupitia kufuatia mapinduzi ya amani.

Katika wakati ambapo mjumbe wa serikali kuu anaeshughulikia masuala ya mashariki, Christian Hirte anasifu ufanisi uliopatikana tangu Ujerumani mbili zilipoungana upya, waziri mkuu wa jimbo la Schleswig Holstein Daniel Günther wa chama cha CDU ametilia mkazo umuhimu wa juhudi za pamoja ili kuepusha usitokee tena ufa kati ya Mashariki na Magharibi."Licha ya maendeleo makubwa ,katika maeneo mengi ya majimbo mepya bado kuna hali ya ya kutoridika na watu kujihisi wanyonge anasema mwakilishi wa serikali kuu katika maeneo ya Mashariki,Christian Hirte.

Rais Vladimir Putin wa UrusiPicha: picture-alliance/AA/Russian Presidential Press and Information Office

Vladimir Putin aelezea matumaini ya kuimarishwa ushirikiano kati ya Urusi na Ujerumani

Katika daraja ya kimataifa muungano wa Ujerumani unasifiwa. Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameutaja kuwa tukio la kihistoria lililomaliza Vita Baridi barani Ulaya. Katika risala yake ya pongezi kwa rais wa shirikisho Frank-Walter Steinmeier na Kansela Angela Merkel, kiongozi huyo wa Urusi amesema tunanukuu "Kwa kuungana upya Ujerumani, umefunguka ukurasa mpya katika uhusiano wa mataifa yetu mawili". Putin ameelezea matumaini yake kuona ushirikiano ukinawairi katika sekta mbalimbali kati ya Ujerumani na Urusi.

Sherehe za miaka 30 ya muungano zitaendelea hadi usiku mjini Kiel na katika miji mengine pia ya Ujerumani.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/epd/dpa/AFP/KNA/

Mhariri: Grace Patricia Kabogo

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW