Sheria ya kiislam kutumika katika bonde la Swat nchini Pakistan
24 Februari 2009Wapiganaji wa Taliban nchini Pakistan wametangaza usimamishaji mapigano wa kudumu katika bonde la Swat,kaskazini magharibi ya nchi hiyo.
Mpango huo wa kuweka chini silaha umefuatia makubaliano ya kuanza kutumika sheria ya kiislam ,kama mfumo pekee wa sheria,katika bonde hilo la milima ya Himalaya.
Mpango huo wa kuweka chini silaha unatishia kuzidisha wasi wasi wa nchi za magharibi,zinazohofia Pakistan isije ikageuzwa ngome ya wanaharakati wa kiislam.
Matumizi ya nguvu katika bonde la Swat,yaliyoripuka mwishoni mwa mwaka 2007 yaligharimu maisha ya zaidi ya watu 1200.
""Tumekubali kuweka chini silaha kwa muda usiokua na mwisho" amesema hayo msemaji wa wataliban-Muslim Khan,hii leo.
Wataliban wa bonde la Swat waliamua kwa mara ya kwanza kuweka chini silaha kwa muda wa siku 10,February 15 iliyopita.Siku ya pili yake,kiongozi mashuhuri wa kidini katika eneo hilo Maulana Sufi Mohammad akapata ridhaa ya viongozi wa serikali, sheria ya kiislam itatumika katika eneo hilo ikiwa matumizi ya nguvu yatakoma daima.
Waasi wanaoongozwa na Maulana Fazlullah,mkwe wa Sufi Mohammad,wameamua kuwaachia huru wafungwa wanne hii leo,wakiwemo wanasiasa wawili.Wameahidi pia kuwaachia wafungwa wote bila ya masharti,wanasema.
Jana jeshi la Pakistan lilisema linasitisha opereshini za kijeshi dhidi ya wataliban katika eneo hilo.
Malaki ya watu wameyapa kisogo maskani yao katika bonde la Swat,linalodhibitiwa kwa sehemu kubwa na waasi licha ya kuwepo vikosi vinne vya wanajeshi wasiopungua 16 elfu.
Kwa miaka sasa,wamarekani,na nchi za magharibi wamekua wakiishinikiza serikali ya mjini Islamabad izuwie harakati za wafuasi wa itikadi kali ya dini ya kiislam katika ardhi yake na hasa katika maeneo yanayopakana na Afghanistan ambako wataliban na Al Qaida wanaandaa hujuma zao bila ya shida dhidi ya Afghanistan.
Msemaji wa jeshi la Pakistan amesema waasi hawatakua tena na njia katika bonde la Swat litakapokua linadhaminiwa na serikali.