Sheria ya kupinga LGBTQ Iraq yakosolewa na wanaharakati
28 Aprili 2024Mashirika ya kutetea haki za binadamu na wanadiplomasia wamekosoa sheria iliyopitishwa na bunge la Iraq mwishoni mwa juma hili, ambayo itatoa adhabu kali ya hadi miaka 15 jela kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja na wale wanaobadili jinsia.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Matthew Miller, amesema katika taarifa yake kwamba sheria hiyo inatishia watu walio hatarini katika jamii ya Wairaq na inaweza kutumika kubinya uhuru wa kujieleza.
Naye waziri wa mambo ya nje wa Uingereza David Cameron ameitaja sheria hiyo kuwa hatari na ya kuogofya. Ingawa masuala ya mapenzi ya jinsia moja ni mwiko katika jamii ya wahafidhina wa Iraq, nchi hiyo haikuwa na sheria inayotoa adhabu dhidi ya vitendo vya mapenzi ya jinsia moja.
Muswada uliopita, ulikuwa umependekeza adhabu ya kifo kwa watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.