Sheria ya makosa ya mtandao yaanza Tanzania
1 Septemba 2015Akiongea na DW jijini Mwanza nchini Tanzania mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari za uhalifu na dawa za kulevya nchini Tanzania OJADACT, Edwin Soko, amesema kitendo cha serikali kupuuza maoni ya wadau wa habari juu ya baadhi ya vipengele vya sheria hii ni mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa habari nchini.
Ameyataja maeneo yanayopigiwa kelele ni pamoja na kifungu cha 7(2b) kinachosema Mpokeaji wa Ujumbe anaweza kushtakiwa kwa kosa la kupokea ujumbe ambao sheria imeufanya kuwa jinai. “Mfano mtu akikutumia ujumbe aliotumiwa na wewe ukaupokea na wewe uliyeupokea utakuwa umefanya kosa la jinai”alisema Soko.
Maeneo mengine ambayo Soko ameyabainisha ni kifungu cha 21(1), ambacho ameeleza kinamuweka katika mazingira ambayo si salama mtumiaji wa vituo vya mtandao kutokana na kifungu hiki kumtaka mtoa huduma za mtandao kutoa habari zake pale serikali itakapozihitaji.
Wadau wakosoa ukali wa adhabu
Ameongeza kuwa kifungu cha 8 kinaongeza mbinyo wa uhuru wa habari kutokana na kumtaka mtumiaji wa taarifa kutotoa taarifa zenye tafsiri ya usiri kwa umma hata kama ni nyaraka za kusaidia nchi kwa ujumla, sheria inawabinya wananchi kutoa taarifa zenye maslahi kwa umma. “Kifungu hiki kinazuia mtu kutoa taarifa hata kama ni za matumizi mabaya ya mali za umma ikiwa serikali itasema hizo ni taarifa za siri,” aliongeza Soko.
Wadau wa habari wamekosoa vipengele vya adhabu kwa kuweka kiwango cha chini cha adhabu huku kikiwa kimya juu ya ukomo wa adhabu. “Rejea adhabu ya ibara mbalimbali, sheria hii kila kosa linaweza fanya mtu afungwe kifungo hadi maisha na kulipa pesa hadi zisizohesabika kwani hakijaweka kikomo cha juu cha adhabu bali kikomo cha chini tu kwa kiingereza not less than” amefafanua zaidi Soko.
Tafsiri ya taarifa ya ukweli na uhakiki wa taarifa ya mtandaoni
Kuhusu ukweli wa taarifa, Soko anasema kifungu cha 22 kinazidisha mbinyo kutokana na kuainisha kuwa ukiweka ujumbe katika mitandao ya kijamii na ukaufuta au kuuboresha kama ujumbe ukikutwa na kosa, mashataka yataongezewa kosa lingine la kuuboresha ujumbe ama kuufuta.
Kwa upande wake mmiliki wa mtandao wa kijamii wa “BLOG cha Binagi Media Group” George Binagi amesema kuwa utekelezwaji wa sheria hii unazidisha hofu kwa watumiaji wa mitandao kutokana na uwepo wa vifungu vya 31 mpaka 35 na 39 mpaka 45 ambavyo vinaelekeza kuwa mmiliki wa mtandao wa kijamii u mtoa huduma, pale anapobaini kosa na akalitoa na akawa kwenye mkakati wa kuitaarifu mamlaka husika, askari nae anaweza kwa wakai huo huo akaamuru kumkagua na hata kuchukua vifaa vya mwandishi wa mtandaoni ama mmiliki wa kituo cha utoaji wa habari ili kufanya ukaguzi bila amri ya mahakama.
Hofu kwa waandishi wa habari
Kwa upande wake mwandishi wa habari za magazeti nchini Tanzania Baltazar Mashaka kutoka gazeti la kila siku la Jambo Leo, amekosoa baadhi ya vipengele hivyo hususani nguvu kubwa ya kufanya tafsiri ya taarifa ya ukweli na ya uongo.
Serikali inaturudisha kwenye sheria kandamizi za usalamawa taifa ya mwaka 1970 na ile ya magazeti ya mwaka 1976 ambazo tumekuwa tunazilalamikia kila siku kutokana na kuwabinya waandishi wa habari wanapopata taarifa ambazo serikali haitaki zitoke hata kama zinahusu matumizi mabaya ya mali za umma.
Mwandishi: Dotto Bulendu
Mhariri: Elizabeth Shoo