1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria za haki miliki ziondolewe kwa chanjo ya COVID-19

Daniel Gakuba
10 Desemba 2020

Mashirika ya Human Rights Watch na Amnesty International yamezihimiza serikali kutozuia kibali cha muda cha kukiuka sheria zinazolinda haki miliki kuhakikisha chanjo dhidi ya COVID-19 inawafikia wanaohitaji kote duniani

Coronavirus | Impfstoff
Picha: Robin Utrecht/picture alliance

Wito huo wa Human Rights Watch na Amnesty International umekuja wakati Uingereza ikiwa tayari imeanza kutoa chanjo ya COVID-19 kwa watu wake, huku nchi nyingine kadhaa zikitarajiwa kuanza kutoa huduma hiyo pia hivi karibuni.

Katika mkutano wa Shirika la Biashara Duniani-WTO unaofanyika leo mjini Geneva, Uswisi, nchi zinazoshiriki zitajadili pendekezo na India na Afrika Kusini, kutaka kibali cha kukiuka baadhi ya vipengele vinavyolinda haki miliki na masuala mengine yanayohusiana na haki hizo. Ikiwa hili litakubaliwa, litarahisisha upatikanaji wa teknolojia na kurahisisha usambazaji wa chanjo na dawa za kutibu maradhi ya COVID-19, tena kwa bei ambao serikali nyingi duniani zinaweza kuimudu.

Tayari mataifa tajiri yamekwishasaini mikataba ya kununua viwango vikubwa vya dozi za chanjo zitakazotengenezwa mwaka ujao wa 2021, na hatua inayoweza kuchukuliwa mjini Geneva leo yumkini itazisaidia nchi masikini nazo kuweza kupata chanjo hiyo kwa ajili ya watu wao.

Picha: picture-alliance/dpa, Getty Images

Bruno Stagno Ugarte, naibu mkurugenzi mkuu wa Human Rights Watch anayehusika na utetezi wa haki za binadamu, amesema pendekezo la India na Afrika Kusini linalenga kuzisaidia serikali za mataifa kukabiliana na changamoto ya kiafya isiyo ya kawaida, ambayo inaisibu dunia. Aidha, afisa huyo amezisihi serikali katika mkutano wa Geneva kutopoteza muda katika kuidhinisha pendekezo hilo, kwa sababu hilo litasaidia upatikanaji wa dawa na chanjo ambavyo vinahitajika kuokoa maisha ya watu.

Pendekezo laungwa mkono

Kenya, Eswatini, Msumbiji na Pakistan zimeungana na India na Afrika Kusini kulidhamini pendekezo hilo, ambalo tayari limeungwa mkono na nchi nyingine 100, nyingi zikiwa katika kundi la kipato cha chini na cha kati. Hata hivyo, kundi dogo la nchi tajiri na washirika wao wa kibiashara limelipinga pendekezo hilo la kuomba kibali kukiuka baadhi ya sheria za haki miliki. Hizo ni pamoja na Brazil, Canada, Marekani, Uingereza pamoja na Umoja wa Ulaya.

Mshauri wa Amnesty International anayeshughulikia haki ya watu kupata huduma za afya Tamaryn Nelson amezitahadharisha nchi hizo zinazopinga, akisema njia pekee ya kulishinda janga la COVID-19, ni kwa serikali zote kutambua majukumu yao ya kuhakikisha kuwa wale walio na mahitaji zaidi ya kupata chanjo ya kuyanusuru maisha yao, hawasahauliki.

Ameongeza kuwa kuridhia pendekezo la India na Afrika Kusini, itakuwa njia ya kudhihirisha kujitolea kwa mataifa kufanya lolote linalohitajika kulinda uhai wa mabilioni ya watu, bila kujali wanakoishi.

(HRW press release https://bit.ly/37PJmw2)