1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SHEVARDNADZE AJIUZULU GEORGIA

24 Novemba 2003

Kwa maneno yafuatayo:"Naona kuwa mambo hayawezi kuendelea namna hii.Ikiwa kesho nitalazimika kutumia mamlaka yangu,basi kutatokea mmuagiko mkubwa wa damu.Kamwe sijawahi kuisaliti nchi yangu na kwa hivyo ni bora kuwa rais ajiuzulu." ndio Eduard Shevardnadse alivyotangaza uamuzi wake wa kujiuzulu kama rais wa Georgia,ingawa hapo awali alingángania kubakia madarakani.

Tangazo la kujizulu kwa Shevardnadze lilipokewa kwa shangwe na furaha kubwa na maelfu ya wakaazi wa Georgia waliomiminika kati kati ya mji mkuu Tbilisi wakipiga muziki na kucheza barabarani wengine wakiripua fataki.Kwani kwa zaidi ya majuma matatu kwa mfululizo wananchi kwa maelfu na elfu,waliandamana nje ya bunge kumshinikiza Shevardnadse aondoke madarakani wakimtuhumu kuwa alifanya udangányifu katika uchaguzi wa bunge mapema mwezi huu.Hatimaye ni nchi jirani Russia iliojitolea kuwa mpatanishi kutafuta suluhisho kwa mzozo huo uliosababisha hali ya wasi wasi katika jumuiya ya kimataifa,hasa ikiwa ni katika nchi zilizopakana na Georgia.Russia iliyokuwa ikitazama jinsi jungu likitokota nchini Georgia ilimtuma waziri wake wa kigeni Igor Ivanov kutafuta njia ya kuusuluhisha mzozo huo kwa usalama.Ivanov siku ya jumapili alifuatana na viongozi wa vyama vya upinzani Mikhail Saakashvili na Zurab Zhvania kuonana na Shevardnadse nyumbani kwake,ukingoni mwa mji mkuu Tbilisi.Ni baada ya kuwa na mazungumzo hayo ndio lilitolewa tangazo la kujiuzulu kwa Shevardnadze ambae wakati wa enzi ya Soviet Union,alikuwa waziri wa kigeni katika serikali ya Moscow.Lakini mnamo mwaka 1990 Schevardandse alijiuzulu kama waziri wa kigeni akionya kuwa nchi hiyo iliyokuwa ikisambaratika ilianza kuwa na uongozi wa kidikteta.Schevardnadse daima alijaribu kuzuia utumizi wa mabavu na amesifiwa kuwa ni yeye alierahisisha utaratibu ulioziwezesha nchi za Ulaya Mashariki kwa amani,kujitenga na mkono wa chuma wa Moscow.

Na hata serikali za vyama mbali mbali nchini Ujerumani hazikusahau vipi,licha ya kuwepo upinzani kutoka baadhi ya serikali za Ulaya,Schevardnadze aliisaidia Ujerumani kutimiza matumainio ya miaka na miaka ya kutaka kuwa na Ujerumani moja iliyoungana.Serikali ya Gerhard Schroeder mjini Berlin ikikumbuka mchango huo muhimu wa Schevardnadse,imesema kuwa Ujerumani itafurahi kumkaribisha Shevardnadze kwa sababu ya msaada aliotoa kuleta muungano wa Ujerumani.

Kwa kweli hata nchini Georgia,Schevardnadse amesifiwa na wengi kuwa ni yeye ndio alieiokoa nchi hiyo kutoka utawala wa vurugu,aliposhika madaraka hapo mwaka 1992.Lakini sasa nchini Georgia ni yeye anaelaumiwa kuwa ameyatumia madaraka yake visivyo.Baadhi kubwa ya wananchi wanamlaumu Schevardnadze kuwa ameitumbukiza nchi katika hali mbovu ya kiuchumi. Ingawa hali ya uchumi nchini Georgia ni mbaya sana,nchi hiyo inatazamwa kwa hamu na madola ya magharibi kwani kuna bomba la mafuta linalojengwa kusafirisha mafuta kutoka eneo la Caspian hadi Bahari ya Kati,bomba hilo likipitia nchini Georgia.Lakini matokeo ya nchini Georgia bila ya shaka yatasababisha hali ya wasi wasi miongoni mwa viongozi wa nchi ambazo zamani zilikuwa sehemu ya Soviet Union.Kwani viongozi wengi wa nchi hizo walipanda juu,enzi za Soviet Union,kabla ya nchi hizo kuwa na uhuru wao,na wengi wao hutawala kwa mkono wa chuma.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW