1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maafisa saba wa Umoja wa Mataifa wafukuzwa Ethiopia

1 Oktoba 2021

Marekani yasema itaiwekea vikwazo Ethiopia baada ya serikali ya nchi hiyo kuwafukuza maafisa saba wa mashirika ya kutoa misaada ya Umoja wa Mataifa ambao wanadaiwa kujihusisha na maswala ya ndani ya nchi hiyo.

Symbolbild I UN I Äthiopien
Picha: Albert Gonzales Farran/AFP/Getty Images

Wizara ya mambo ya nje ya Ethiopia imewapa maafisa saba wa Umoja wa Mataifa muda wa saa 72 kuondoka Ethiopia kwa kile ambacho serikali ya nchi hiyo imedai wamejiingiza katika mambo ya ndani ya ya nchi hiyo. Wakati huo huo shinikizo linaongezeka dhidi ya serikali ya Ethiopia kuhusu jimbo la Tigray.

Serikali ya Ethiopia imechukua uamuzi wa kuwafukuza maafisa hao wa Umoja wa Mataifa baada ya wafanyakazi wa kutoa misaada kutanabahisha juu ya hali ya maafa katika jimbo la Tigray inayotokana na kushindikana kupeleka misaada kwenye sehemu hiyo. Miongoni mwa maafisa hao saba wa mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa wanoatakiwa kuondoka nchini Ethiopia ni pamoja na naibu mratibu wa misaada nchini humo Grant Leaty na mwakilishi wa shirika la watoto la UNICEF, Adele Khodr. 

Mwakilishi wa UNICEF Adele KhodrPicha: Rahmat Alizadah/Xinhua News Agency/picture alliance

Umoja wa Mataifa umesema hatua ya kuwafukuza maafisa wake kutoka nchini Ethiopia inahatarisha zaidi ufikishaji wa misaada ya kibinadamu katika mkoa wa Tigray ulio na watu wapatao milioni 6 na unaokumbwa na mgogoro kwa karibu mwaka mmoja sasa. Umoja wa Mataifa umesema shughuli za kupeleka vifaa vya matibabu, chakula na mafuta zimesimama.

Msemaji msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Stephanie Tremblay, amesema Umoja wa Mataifa utaendelea kuziangazia shida zinazowakabili watu wa jimbo la Tigray.

Serikali ya Ethiopia imewashutumu wafanyikazi wa Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono vikosi vya Tigray ambavyo vimekuwa vikipambana na wanajeshi wa serikali ya shirikisho na vikosi vya washirika wake tangu mwezi Novemba mwaka uliopita. Wafanyikazi hao wamekana shutuma hizo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada, Martin Griffiths, wiki hii aliliambia shirika la habari la The Associated Press (AP) kwamba mgogoro nchini Ethiopia ni doa kwa dhamira ya ubinadamu kwa kuwa watoto na watu wengine wanakufa kwa njaa katika jimbo la Tigray kutokana na serikali kuzuia misaada. Watu wapatao 400,000 wanakabiliwa na hali mbaya ya njaa.

Vyanzo:RTRE/AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW