Shinikizo laongezeka kumtaka Zuma ajiuzulu
6 Aprili 2016Muungano wa makanisa, wanataaluma pamoja na mashirika mengine, yameanzisha kampeni dhidi ya Rais Zuma, ambaye ameomba radhi na kukiri kosa baada ya mahakama ya juu ya Afrika Kusini kutoa uamuzi kuwa kiongozi huyo alikiuka katiba kwa kutumia mamilioni ya Dola, katika fedha za umma kwa ajili ya kuyafanyia ukarabati makaazi yake binafsi.
Muungano huo umesema utajadili mipango yake baadae leo. Waziri wa zamani wa fedha wa Afrika Kusini, Trevor Manuel na Ahmed Kathrada, mwanaharakati mkongwe dhidi ya ubaguzi wa rangi na aliyekuwa rafiki wa karibu wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela, wamemtaka Rais Zuma ajiuzulu wadhifa wake.
Bunge la Afrika Kusini ambalo limetawaliwa na wanachama wa chama tawala cha African National Congress-ANC, hapo jana lilipiga kura kupinga hoja ya upinzani ya kumuondoa madarakani Rais Zuma, kutokana na kashfa ya rushwa iliyokuwa inamkabili. Wabunge 233 walipiga kura kupinga hoja hiyo, huku wabunge 143 wakipiga kura kuunga mkono hoja, kwa sababu hawana imani naye. Hakuna mbunge yeyote ambaye hakupiga kura.
Hoja iliwasilishwa bungeni na chama cha upinzani
Hoja hiyo ilipelekwa bungeni na chama cha upinzani cha Democratic Alliance-DA, baada ya uamuzi uliotolewa wiki iliyopita na Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini. Mbunge wa ANC, John Jeffery ameliambia bunge kwamba uamuzi uliotolewa na mahakama haukutoa sababu za mjadala kuhusu kuondolewa Zuma madarakani. Hata hivyo, kiongozi wa chama cha DA, Mmusi Maimane, amesema kuwa suala la rushwa limekiathiri chama chote cha ANC, kama saratani.
''Kwa kweli ni aibu sana kwamba bunge limevunja tena sheria sawa na hiyo. Sisi kama wapinzani hatuwezi kukaa hapa pamoja na chama kisichofata taratibu za kikatiba. Lazima tueleweke wazi kwamba hatutakubaliana na makosa ya kuipindua demokrasia ya taifa letu. Hapana haiwezekani kuwa hivyo spika,'' alisema Maimane.
Mchakato huo ulionekana kama pigo kwa Zuma, ambaye amekuwa rais wa kwanza wa Afrika Kusini kukabiliwa na mjadala bungeni wa kutokuwa na imani naye. Imeripotiwa kwamba Rais Zuma ambaye amenusurika hoja ya kushtakiwa, alitumia kiasi cha Dola milioni 16 ambazo ni fedha za umma kukarabati makaazi yake binafsi kwenye mji wa Nkandla.
Rais Zuma alidai kuwa amezitumia fedha hizo za walipa kodi kwa kufanya ukarabati ambao ulihusisha bwawa la kuogelea, eneo la mifugo, mabanda ya kufugia kuku, kituo cha wageni pamoja na eneo la kufanyia burudani.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AP,DPA,RTR,AP
Mhariri: Iddi Ssessanga