1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miili ya mateka 19 wa Israel bado kizungumkuti

17 Oktoba 2025

Hali ya utulivu imeendelea kushuhudiwa kwenye kanda ya Mashariki ya Kati kufuatia makubaliano ya kusitisha vita yaliyotiwa saini mapema wiki hii.

Israel, mji wa Petah Tikva
Familia za mateka nchini Israel zinataka serikali ilishinikize kundi la Hamas kuikabidhi miili ya jamaa zao. Picha: Stoyan Nenov/REUTERS

Hata hivyo, mvutano kuhusu utekelezaji wa mkataba huo unatishia kurejesha uhasama kati ya Israel na kundi la Hamas. Hali hiyo inatokana na shinikizo linaloongezeka ndani ya Israel la kuitaka Hamas itekeleze masharti ya mkataba hususani kurejesha miili yote ya mateka wa Israel.

Chini ya makubaliano ya kusitisha vita, kundi hilo lilitakiwa kuwaachia huru mateka wote walio hai na kukabidhi miili ya wale waliouawa au kufa wakiwa kizuizini. 

Tangu utekelezaji ulipoanza, mateka 20 wa Israel walikwishaachiwa na miili ya 9 kati 28 ilikabidhiwa. Hamas imesema miili ya mateka wengine 19 bado haijapatikana na inashindwa kuifikia kutokana na kukosa vifaa vya kupekua vifusi kwenye Ukanda wa Gaza.

Mvutano huo umeyaweka rehani makubaliano ya kusitisha vita hasa baada ya viongozi wa Israel kuionya Hamas kuwa mapigano yataanza tena iwapo miili hiyo haitopatikana na kukabidhiwa.

Waziri Mkuu wa Israel alisema jana Alhamisi kwamba amedhamiria "kuipata miili ya mateka wote". 

Hasira zinaongeza miongoni mwa familia za mateka wanaotaka angalau kupata miili ya ndugu na jamaa zao. Familia hizo zimeitaka serikali isitishe "mara moja utekelezaji wa hatua ziantofuata za mkataba wa kusitisha vita hadi pale Hamas itakapotimiza wajibu wake wa kukabidhi miili" ya wapendwa wao.

Hapo jana Uturuki ilichukua jukumu la kusaidia zoezi la utafutaji miili hiyo kwa kutuma kikosi cha waataamu kufukua na kupekua vifusi ndani ya Ukanda wa Gaza.

Israel yahimizwa kufungua milango kuruhusu misaada Ukanda wa Gaza 

Malori yenye misaada ya kibinadamu kwenye kivuko cha Rafah.Picha: Amr Abdallah Dalsh/REUTERS

Katika hatua nyingine miito imeongezeka kuitaka Israel iruhusu misaada ya kiutu kuingia Ukanda wa Gaza kwa kufungua vivuko vya mipakani hususani kile cha Rafah kinachoitenganisha Gaza na Misri.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Israel Gideon Saar amesema tayari matayarisho yanaendelea na kivuko hicho huenda kitafunguliwa siku ya Jumapili.

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetahadharisha kwamba magonjwa ya mlipuko na yale ya kuambukiza yanasambaa kwa kasi ndani ya Gaza ambayo haina idadi ya kutosha ya hospitali au vituo vya afya.

Mkuu wa WHO kwenye kanda hiyo Hanan Balkhy amesema homa ya uti wa mgongo, ugonjwa wa kuhara na maradhi ya mfumo wa njia ya kupumua vinatishia usalama wakaazi wa Gaza.

Wakati hayo yakiarifiwa, Ufaransa na Uingereza zimesema kwa kushirikiana na Marekani zinakamilisha azimio litakalounda kikosi cha kimataifa cha askazi kitakachopelekwa Gaza.

Azimio hilo litawasilishwa mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kupigiwa kura. Kikosi hicho kitakuwa na jukumu la kusimamia usalama ndani ya Gaza.

Marekani amearifu kuwa inawasiliana na serikali kadhaa duniani zilizoonesha utayari wa kuchangia askari wa kikosi hicho kitakachokuwa na muundo sawa na kile kilichotumwa nchini Haiti.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW