Shinikizo laongezeka kwa viongozi wa jimbo la Catalonia
20 Oktoba 2017Vyama vya kisiasa nchini Uhispania vinashinikiza kufanyike uchaguzi kwa sababu vinapendekeza kuwa hiyo ndio njia pekee ya kuinusuru nchi hiyo kutoka kwenye mgogoro mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini Uhispania katika kipindi cha miongo mingi. Chama cha upinzani cha Kisoshalisti kimesema kinaunga mkono hatua zozote zitakazochukuliwa na serikali kuu dhidi ya mamlaka ya jimbo la Catalonia ambalo kitisho chake cha kutaka kujitenga kimesababisha mtafaruku katika sarafu ya Euro ambao umeathiri hali ya uchumi wa jimbo hilo la nne kwa utajiri wa katika eneo la Umoja wa Ulaya. Waziri mkuu wa Uhispania Mariano Rajoy amesema utawala wa jimbo la Catalonia umekiuka sheria.
Waziri mkuu wa Uhispania Mriano Rajoy aliutaka upinzani ushirikiane naye ili aweze kuwasilisha msimamo wa pamoja dhidi serikali ya jimbo la Catalonia. Rajoy hapo kesho anatarajiwa kufanya mkutano maalum wa baraza la mawaziri ili kuuanzisha mchakato huo wa kuweka sheria ya lazima. Itakuwa ni mara ya kwanza tangu Uhispania kuingia katika demokrasia miongo minne iliyopita kuainisha ibara ya 155 ya katiba ya nchi hiyo inayoipa nguvu serikali kuu kuipokonya mamlaka serikali ya jimbo na kuitisha uchaguzi mpya. Waziri mkuu anataka aungwe mkono kwa kiwango kikubwa kabla ya kuichukua hatua hiyo ambayo imeongeza wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokea maandamano makubwa katika jimbo la Catalonia.
Wateja wa benki
Wakati mgogoro wa kisiasa ukiendelea nchini Uhispania wateja wa mabenki wanaendelea kutoa fedha zao kwenye benki ambazo zimehamisha makao yao makuu na kuyapeleka katika sehemu zingine nchini Uhispania. Leo hii wateja wengi walionekana wakiwa wamepanga foleni ndefu wakisubiri kutoa fedha. Benki za CaixaBank na Banco Sabadel ambazo ndio wakopeshaji wakubwa katika jimbo la Catalonia ni miongoni mwa taasisi za kifedha zilizohamisha biashara zao kutoka katika jimbo hilo la Catalonia. Kiongozi wa jimbo la Catalonia Carles Puigdemont ameshikilia msimamo wake bado anasema iwapo hakutakuwepo na mazungumzo baina ya upande wake na serikali atatangaza uhuru wa jimbo lake hilo.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/AFPE/RTRE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman