Shinikizo lazidi kuongezeka kumtaka Bouteflika ajiuzulu
27 Machi 2019Kauli ya Jenerali Salah imetolewa baada ya maandamano ya umma yaliyodumu kwa zaidi ya mwezi mmoja yakimtaka Bouteflika aondoke madarakani baada ya kuiongoza Algeria kwa miaka 20. Akizungumza kupitia televisheni ya Algeria, Salah amesema hilo ndilo litakuwa suluhisho pekee la kuleta utulivu wa kisiasa nchini humo.
''Nchi yetu imeshuhudia maandamano ya amani, watu wakitaka mabadiliko ya kisiasa. Hivyo nawaomba wote tuonyeshe uzalendo kwa maslahi ya taifa letu. Suluhisho litakalosaidia kupatikana kwa utulivu wa kisiasa ni kupitia katiba ambayo tunaiheshimu. Suluhisho ni kutumia kifungu cha 102 cha katiba ya Algeria,'' alisema Salah.
Ombi kwa bunge
Kiongozi huyo wa kijeshi amesema chini ya kifungu hicho, Baraza la Katiba linaweza kuamua kwamba rais ni mgonjwa mno na hawezi kutekeleza majukumu yake na ameliomba bunge la Algeria kumtangaza Bouteflika kuwa ni mtu asiye na uwezo tena.
Kulingana na katiba ya Algeria, iwapo ombi hilo litakubaliwa kwa wingi wa theluthi mbili na wabunge wa nchi hiyo, Spika wa Bunge atachukua madaraka ya serikali hadi uchaguzi wa rais utakapofanyika.
Wakati hayo yakijiri, kiongozi wa chama cha Democratic National Rally, RND Ahmed Ouyahia amemtaka Rais Bouteflika kujiuzulu. Chama hicho ni moja kati ya vyama vinavyounda serikali ya muungano inayotawala Algeria na ambacho kina ushawishi mkubwa na kilichokuwa kikimuunga mkono Boutelfika kwa muda mrefu.
Ouyahia aliyekuwa waziri mkuu wa Algeria, amesema chama hicho kinamtaka kiongozi huyo ajiuzulu kulingana na kifungu cha 102 kilichopo kwenye aya ya nne ya katiba ya Algeria, ili kuruhusu kipindi cha amani cha mpito.
Baadhi ya waandaamanaji walitoa wito wa kutumika kwa kifungu cha 102 kwa lengo la kumuondoa Bouteflika madarakani, tangu Februari 22, yalipoanza maandamano ya kila Ijumaa ya kuupinga utawala wa wake. Maandamano hayo yamekuwa yakiungwa mkono na chama cha RND pamoja na Chama tawala cha National Liberation Front, FLN.