Shinikizo lazidi kwa Saudia juu ya kupotea kwa Kashoggi
9 Oktoba 2018Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan amewataka maafisa wa Saudi Arabia kuthibitisha madai yao kwamba mwandishi wa habari na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Riyadh ambaye hajulikani alipo, Jamal Kashoggi aliondoka kwenye ubalozi huo mdogo, katika wakati ambapo Marekani na Umoja wa Mataifa wakitaka uchunguzi wa kina kuhusu kupotea kwake.
Amesema "Ni lazima tufikie tamati mapema iwezekanavyo, na maafisa wa ubalozi wa Saudi hawawezi kujitetea kwa kusema tu kwamba aliondoka ubalozini. Mamlaka husika zinatakiwa kuthibitisha madai ya suala hili".
Rais Recep Tayyip Erdogan, ametoa matamshi haya akiwa jijini Budapest baada ya vyombo vya habari hapo jana kuripoti serikali yake imeomba kibali kwa Saudi Arabia cha kupekua makazi ya ubalozi huo mdogo uliopo mjini Instanbul.
Kashoggi, alipotea Jumanne iliyopita baada ya kuingia kwenye ubalozi huo mdogo, ili kuchukua nyaraka, kwa ajili ya maandalizi ya harusi yake na mchumba wake raia wa Uturuki.
Rais Donald Trump wa Marekani amesema ana wasiwasi na kupotea kwa mwandishi huyo, anayedaiwa kuuawa kwenye ubalozi huo mdogo wa Saudi Arabia. Na alipozungumza na waandishi wa habari katika ikulu ya White House akasema, "Nina wasiwasi. Sipendi kusikia taarifa hizi. Ninaamini kwamba watalipatia ufumbuzi. Kwa sasa hakuna anayejua kuhusu hili, kuna taarifa mbaya zinasambaa. Sizipendi."
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo, kwenye taarifa iliyotolewa usiku wa jana ameitaka serikali ya Saudi Arabia kusaidia uchunguzi wa kina wa kupotea kwa Kashoggi.
Jana Jumatatu, waandamanaji walikusanyika nje ya ubalozi huo mdogo wakiwa na mabango yaliyoandikwa hatuondoki bila ya Kashoggi, wakishinikiza kuambiwa kuhusu kile kilichomtokea. Mwanaharakati, raia wa Yemen Tawakkol Karman, aliyeshinda tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2011, alisema utakuwa ni uhalifu wa kutisha, iwapo madai hayo ya mauaji yatakuwa na ukweli.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres naye pia ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu kupotea kwa Kashoggi, lakini pia unyanyasaji dhidi ya waandishi wa habari. Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephanie Dujarric amesema, Guterres anafuatilia kwa karibu kisa hicho.
Polisi ya Uturuki ilisema mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba takriban raia 15 wa Saudi Arabia, ikiwa ni pamoja na maafisa waliwasili mjini Instanbul Jumanne iliyopita na walikuwa ndani ya ubalozi, wakati Kashoggi pia akiwa bado hajaondoka. Chanzo kutoka serikali ya Uturuki kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba, polisi wanaamini kwamba mwandishi huyo aliuawa na timu maalumu iliyotumwa Instanbul na ambayo iliondoka mara tu baada ya mauaji hayo.
Saudi Arabia inakana vikali madai hayo, na imeendelea kusisitiza kwamba Kashoggi aliondoka ubalozini hapo.
Mwandishi: Lilian Mtono/ AFPE/DPAE.
Mhariri: Iddi Ssessanga