1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la afya duniani laadhimisha miaka 60

Charo, Josephat7 Aprili 2008

Mada mbiu ni mabadiliko ya hali ya hewa na afya

Margaret Chan mkurugenzi wa shirika la afya duniani WHOPicha: AP

Shirika la afya duniani, WHO, linaadhimisha miaka 60 tangu lilipoanzishwa. Umri wa miaka 60 ni wakati wa kujiandaa kustaafu lakini shirika la WHO linautumiwa umri huu kama mwanzo mpya wa kukabiliana na chamgamoto kubwa ya mabadiliko ya hali ya hewa.

Shirika la WHO lilianzishwa mnamo tarehe 7 mwezi Aprili mwaka wa 1948 baada ya kumalizika vita vya pili vya dunia, wakati ambapo magonjwa ya kuambukiza kama vile kipindupindu yalitishia ulimwengu ambao tayari ulikuwa umedhoofishwa na miaka sita ya mgogoro uliosababisha umwagikaji mkubwa wa damu.

Miaka sitini baadaye shirika la WHO lenye makao yake makuu mjini Geneva nchini Uswisi, lina wanachama 193. Kazi yake kubwa ni kukabiliana na maswala mbalimbali ya afya yakiwemo uvutaji sigara, usalama wa barabarani pamoja na vitisho vya ugonjwa wa ukimwi na homa ya mafua ya ndege.

Mkurugenzi mtendaji wa WHO, Bi Margaret Chan, ameyachagua maadhimisho ya miaka sitini ya shirika hilo kulishughulikia tatizo la mabadiliko ya hali ya hewa na athari zake katika afya ya umma duniani kote.

Shirika la afya duniani linasema mabadiliko ya hali ya hewa yanaweza kusababisha magonjwa kama vile malaria kuenea wakati kiwango cha joto kitakapoongezeka. Ukame na mafuriko yanaweza kuongeza athari kwa afya ya mamilioni ya wahanga duniani kote. Ndio maana mwaka huu shirika la WHO likiadhimisha miaka sitini limechagua mada mbiu isemayo "Mabadiliko ya hali ya hewa na Afya".

David Heymann, naibu mkurugenzi wa shirika la WHO anayesimamia kitengo cha afya, usalama na mazingira anasema mabadiliko ya hali ya hewa yataathiri afya ya binadamu.

"Tayari tumepata picha vipi mabadiliko ya hali ya hewa yatakavyoathiri dunia yetu hii katika afya ya umma kama vile hewa safi, maji salama na chakula. Kwa hiyo mabadiliko ya hali yahewa yanadhihirisha wazi kwamba afya ya umma itaathirika sana."

Magonjwa yanayopatikana katika nchi za joto kama vile malaria yanaenea kwa kasi kuelekea eneo la kaskazini la dunia kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Bwana Heymann anasema nchi maskini zitaathirika zaidi.

"Nchi zinazoendelea na hususan nchi maskini duniani, zitaathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa. Idadi ya watu wanaoumwa na mbu itaongezeka kutoka na kuongezeka kwa idadi ya mbu. Idadi ya watu walio na miundombinu mibaya ya afya itaongezeka na watakaoathiriwa wengi watakuwa akina mama na watoto"

Mtoto wa Ethiopia akipewa chanjo dhidi ya ugonjwa wa kupooza. Mifumo ya afya inahitaji kuimarishwaPicha: AP Photo

Shirika la WHO linataka kujengwe mifumo imara ya afya katika nchi zinazoendelea ili kuzuia athari zinazoweza kusababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya ya binadamu. Ili kuweza kufanikisha hilo kunahitajika wafanyakazi wa afya jambo ambalo bwana David Heymann anasema litakuwa na ugumu wake.

"Tatizo litakuwa na sura mbili. Kwanza katika nchi zenyewe wafanyakazi wa afya hupendelea kufanya kazi mijini na maeneo ya mashambani hayawavutii. Kuna tatizo pia la uhamiaji wa wafanyakazi hawa kwenda katika nchi za kigeni zilizoendelea. Kwa hiyo kutakuwa na matatizo mawili yatakayoimarisha tatizo la utoaji huduma za afya katika miongo ijayo kwa sababu ya kuzorota kwa mifumo ya afya na mipango ya kuangamiza mbu."

Shirika la WHO limebaini kuwa kuna uhusiano kati ya mabadiliko ya hali ya hewa na magonjwa. Bila ushirikiano magonjwa kama vile kipindupindu, malaria na homa ya matumbo yataenea kwa kasi kubwa duniani kote. Bwana Heymann anasisitiza haja ya nchi zilizoendelea kujenga na kuboresha mifumo ya afya duniani.

"Tuna ushahidi katika sekta ya afya kwamba kutakuwa na athari kubwa za mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya ya umma. Tunahitaji kuufikisha ujumbe huu kwa waundaji sera katika nchi mbalimbali kupitia siku ya afya duniani na mkutano wa baraza kuu la shirika la afya duniani, WHO"

Mkutano wa baraza kuu la shirika la afya duniani utakaofanyika baadaye mwaka huu utajadili azimio kuhusu athari za mabadiliko ya hali ya hewa kwa afya, haja ya kuimarisha mifumo ya afya, kufanya utafiti unaohitajika kuendeleza teknolojia, kutabiri na kutathimini athari za mabadiliko ya hali ya hewa na maswala yote yatakayoufanya mfumo wa afya duniani kuwa imara.