1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

260510 AI Jahresreport 2010

Josephat Nyiro Charo27 Mei 2010

Shirika la Amnesty International limeupongeza mwaka jana 2009 kama mwaka muhimu kuhusu haki kwenye ripoti yake iliyotolewa jana. Shirika hilo limesema maafisa wa usalama barani Afrika waliua bila hofu ya kuadhibiwa

Claudio Cordone, katibu mkuu wa Amnesty InternationalPicha: AP

Kwenye ripoti ya mwaka 2010 kuhusu hali ya haki za binadamu ulimwenguni shirika la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, lenye makao yake makuu mjini London Uingereza, limeueleza waranti wa mahakama ya ICC wa mwaka 2009 wa kukamatwa rais wa Sudan Omar al Bashir kujibu mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, kuwa tukio kubwa muhimu linalodhihirisha kwamba hata marais walio madarakani wako chini ya sheria.

Mkuu wa shirika la Amnesty International tawi la Ujerumani, Monika Lüke anasema, "Ufanisi mkubwa ni waranti wa kimataifa wa kukamatwa rais wa Sudan Omar al Bashir mwezi Machi mwaka jana uliotoa ishara kwa wote wanaowatesa na kuwatia gerezani wengine kwamba hawawezi kufanya hivyo bila kuadhibiwa. Ni mara ya kwanza kwa rais aliye madarakani kukabiliwa na waranti ya mahakama ya kimataifa."

Shirika hilo limezitaka serikali mbalimbali kusaini mkataba unaoitambua kikamilifu mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita mjini The Hague Uholanzi ili kuhakikisha uhalifu chini ya sheria ya kimataifa unaweza kushughulikiwa mahala popote duniani. Marekani, Urusi, China, Indonesia na Uturuki ni miongoni mwa mataifa ambayo hayajasaini mkataba huo.

Bi Monika Lüke ameikosoa Urusi, Sri Lanka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa ukiukaji wa haki za binadamu. Ameongeza kwamba hali ya haki za binadamu imeendelea kuwa mbaya nchini Urusi chini ya utawala wa rais Dmitry Medvedev.

Katibu mtendaji wa shirika la Amnesty, Monika Lüke, akiwasilisha ripoti mjini BerlinPicha: picture alliance/dpa

Vikosi vya usalama na maafisa wa polisi barani Afrika wamelaumiwa kwa kuwaua mamia ya watu mwaka jana 2009 lakini hawakuchunguzwa kutokana na utamaduni wa kutojali kuadhibiwa wala kuchukuliwa hatua yoyote.

Ripoti imegusia mauaji ya kiholela yaliyofanywa kwenye uwanja wa michezo katika mji mkuu wa Guinea, Conakry mwezi Septemba mwaka jana ambapo zaidi ya watu 150 waliokuwa wakishiriki kwenye maandamano waliuwawa na wanawake wakabakwa hadharani. Shirika la Amnesty International linasema uhalifu dhidi ya binadamu ulifanyika na kupendekeza kesi hiyo iwasilishwe kwa mahakama ya ICC mjini The Hague.

Shirika hilo limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali nchini Nigeria, likisema mamia ya watu huuwawa kila mwaka mikononi mwa polisi. Cameroon pia imenyoshewa kidole cha lawama huku kukiwa hakuna dalili yoyote ya serikali kuanza kuchunguza mauaji ya watu takriban 100 mnamo mwaka 2008 wakati wa operesheni dhidi ya waandamanaji.

Nchini Kenya, shirika la Amnesty International linasema serikali imeshindwa kuchunguza kikamilifu ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na 2008 ambapo zaidi ya watu 1,000 waliuwawa.

Ripoti pia imeitaja Madagascar ikisema hakuna uchunguzi huru ulioanzishwa kuchunguza mauaji ya watu wasiopungua 31, mnamo Februari 7 mwaka jana wakati wanajeshi wa nchi hiyo walipowafyatulia risasi waandamanaji walipokuwa wakiandamana katika ikulu ya rais mjini Antananarivo.

Huko Zimbabwe hali ya haki za binadamu iliboreka kidogo kufuatia kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa mwezi Februari mwaka jana. Hata hivyo kuteswa na kutishwa kwa watetezi wa haki za binadamu, wanaharakati wa kisiasa na wafuasi wa chama cha upinzani, Movement for Democratic Change, MDC, cha waziri mkuu Morgan Tsvangirani, kuliendelea.

Gereza la Guantanamo bay nchini Cuba

Rais wa Marekani Barack Obama amekosolewa kwa kushindwa kuifunga jela ya Guantanamo Bay nchini Cuba. Wafungwa 198 waliendelea kuzuiliwa katika gereza hilo kufikia mwisho wa mwaka jana licha ya ahadi ya utawala wa Obama kulifunga kufikia Januari 22 mwaka huu.

Iran imekosolewa kwa kuwakandamiza, kuwatesa, kuwakamata na kuwaua waandanaji baada ya uchaguzi wa rais wa mwezi Juni mwaka jana. Maafisa wamekosolewa kwa kubana uhuru wa kujieleza, kuzuia mawasiliano ya simu za mkono na mtandao wa intaneti.

Barani Asia China iliongeza shinikizo dhidi ya wapinzani wa serikali kwa kuwazuilia na kuwatesa wanaharakati wa haki za binadamu. Maelfu ya watu wamekimbia mateso na hali ngumu ya kiuchumi nchini Korea Kaskazini na Myanmar.

Katika mzozo wa Gaza na kusini mwa Israel, vikosi vya Israel na makundi ya wapiganaji wa Palestina waliua kinyume cha sheria na kuwajeruhi raia. Maelfu ya raia wanakabiliwa na mateso na ukiukaji wa haki kutokana na ongezeko la machafuko ya kundi la Taliban nchini Afghanistan na Pakistan.

Mwandishi: Ripperger, Sabine (DW Berlin)/ZPR/Josephat Charo

Mhariri:Abdul-Rahman

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW