Shirika la fedha la kimataifa lamchagua mkurugenzi mpya
27 Septemba 2007Shirika la fedha la kimataifa IMF hii leo linamteuwa mkurugenzi wake mkuu mpya-nafasi inayotazamiwa kumuangukia zaidi waziri wa uchumi na fedha wa zamani wa Ufaransa Dominique Strauss Kahn,kuliko mpinzani wake Josef Tosovsky wa jamhuri vya Tcheki.
Kiongozi wa sasa wa taasisi hiyo ya kimataifa ya fedha,Rodrigo Rato wa Hispania amejiuzulu na anatazamiwa kung’oka madarakani mwishoni mwa mwezi ujao.
Akijibwaga katika mashindano ya kuania wadhifa huo tangu mapema mwezi July uliopita,waziri huyo wa zamani wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 58 amemuacha guzo mpinzani wake wa dakika ya mwisho.Akiungwa mkono na Umoja wa ulaya,Dominique Strauss Kahn ,tangu wiki iliyopita anajivunia pia uungaji mkono wa Marekani –mteja muhimu wa shirika hilo la fedha la kimataifa.
Marekani inadhibiti asili mia 16.79 ya kura ndani ya baraza kuu la taasisi hiyo ya kimataifa.Nazo nchi za Umoja wa ulaya kwa pamoja zinadhibiti asili mia 32.09 ya kura.
Ili kupata ungaji mkono mkubwa zaidi,na hasa katika nchi zinazoinukia,mwanasiasa huyo wa kutoka chama cha kisoshialisti cha Ufaransa alifika takriban katika kila pembe ya dunia na kuonana na wapiga kura wanaoweakilisha nchi 185 wanachama.
“Ni vizuri kuonana na watu ambao unawahitaji wakuchague.”-alisema hayo Dominique Strauss Kahn wiki iliyopita mjini Washington.
Mpinzani wake,mkuu wa benki kuu ya jamhuri ya Tcheki,aliyewahi kua muda mfuopi waziri mkuu nchini mwake na ambae hii leo anasherehekea miaka 57 tangu azaliwe,hajivunii ungaji mkono wa nguvu.Hata kama anajitokeza kama mtetezi wa masilahi ya mataifa yasiyo na nguvu,Josef Tosovsky anaungwa mkono rasmi na Urusi tuu.
“Tunataraji ataungwa mkono kwa wingi na mataifa yanayoinukia” amesema muakilishi wa Urusi katika shirika la fedha la kimataifa Aleksei Mohzin ,wakati wa mahojiano pamoja na shirika la habari la Ufaransa AFP.
Hata kama karata zinaonyesha zimeshachezwa,Bwana Tosovsky,anaeongoza taasisi ya utulivu wa fedha kisiwani Bali,ana sifa ya kutetea masilahi ya nchi zinazonyanyukia katika shirika hilo.
Kwa nchi hizo zilizogeuka injini ya uchumi wa dunia,makubaliano ya kichini chini yaliyofikiwa baada ya vita vikuu, kati ya Marekani na Ulaya kuhusiana na taasisi hizi mbili za Brettons-Woods-makubaliano yanayotazamiwa kuheshimiwa pia safari hii,yanabidi yabatilishwe.
Chini ya makubaliano hayo ya siri,Marekani inamchagua mwenyekiti wa benki kuu ya dunia nazo nchi za Ulaya zinamchagua mkurugwenzi mkuu wa shirika la fedha la kimataifa.
Robert Zoellick alipoteuliwa mwishoni mwa mwezi June kutetea wadhifa wa mwenyekiti wa benki kuu ya dunia,hakukua na mtetezi yeyote aliyesimama kushinfana nae.
Dominique Strauss Kahn anakiri kuna haja ya kulifanyia marekebisho shirika la fedha la kimataifa:Anaasema:
“Nnafikiri hatukujirekebisha vya kutosha na tunalazimika kufanya haraka hivi sasa.Tunabidi tuanze upya.Mie niko tayari kuwajibika.Hadi sasa hakuna mengi yaliyofanywa ndio maana ya kutofaulu.”
Waziri huyo wa zamani wa uchumi na fedha wa Ufaransa,Dominique Strauss Kahn ameahidi akichaguliwa atasalia madarakani kwa kipindi kizima cha miaka mitano-akizisuta hoja eti ana kiu bado cha kuchaguliwa rais nchini mwake.