1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shirika la Haki Duniani: Malawi ilinde haki za binaadamu

1 Julai 2020

Shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu, HRW limemtaka rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera kulinda haki za binaadamu na utawala wa sheria kama alivyoahidi.

Malawi Opposition Lazarus Chakwera
Picha: Reuters/E, Chagara

Shirika la kimataifa la utetezi wa haki za binaadamu la Human Rights Watch limesema Jumatano, kwamba rais mpya wa Malawi Lazarus Chakwera atalazimika kuutumia ushindi wake kama fursa ya kubadilisha rekodi ya taifa hilo katika masuala ya haki za binaadamu. Chakwera alishinda uchaguzi katika kura ya marudio ya Juni 23, kufuatia ushindi wa asilimia 58.57.

Soma zaidi:Chakwera aapishwa rais mpya nchini Malawi

Uchaguzi wa marudio wa urais ulifanyika kufuatia mahakama ya juu zaidi nchini Malawi kubatilisha maamuzi ya mahakama ya kikatiba kwa kufuta matokeo ya awali yaliyokuwa yamempatia ushindi mwembamba rais anayekabiliwa na matatizo lukuki Peter Mutharika katika uchaguzi wa Mei 29, ikiangazia udanganyifu mkubwa na kuagiza uchaguzi mpya katika kipindi cha siku 150.

Mkurugenzi wa Human Rights Watch kusini mwa Afrika Dewa Mavhinga amesema rais Chakwera atatakiwa kuheshimu haki za binaadamu na utawala wa sheria na kuwa masuala muhimu kwenye utawala wake. Amesema rais huyo mpya anahitaji kuyatekeleza kwa vitendo maneno yake kwamba ushindi wake ni ushindi wa demokrasia na haki.

Waandishi wanalengwa Malawi

Wanaharakati wanaofuatilia unyanyasaji kupitia muungano wa mashirika ya utetezi wa haki za binaadamu nchini humo wamesema, kabla ya uchaguzi wa Juni, kuliibuka machafuko yaliyochochewa kisiasa na wahusika hawakukamata. Wamesema walirekodi ongezeko la visa vya machafuko ya wakati wa uchaguzi pamoja na unyanyasaji dhidi ya wanaharakati na wanasiasa wa upinzani.

Taasisi ya vyombo vya habari Kusini mwa Afrika, tawi la Malawi, MISA, Malawi mnamo Mei 31 ilichapisha taarifa ikielezea wasiwasi kwamba waandishi wanazidi kuwa wahanga ya machafuko ya kisiasa katika wakati ambapo taifa hilo lilipokuwa njiani kuelekea kwenye uchaguzi mpya wa rais.

Chakwera alisema kwenye hotuba yake ya uapisho Juni 28 kwamba ushindi wake utafanikisha ndoto ya Malawi mpya kwa kila mmoja, na shirika hilo limesema serikali yake italazimika kuhakikisha haki kwa kila raia zinaheshimiwa, na hususan jamii za pembezoni.

Haki za binadamu changamoto Malawi

Malawi inakabiliwa na kiwango kikubwa cha changamoto katika eneo la haki za binaadamu ikiwa ni pamoja na kukosekana usawa, umasikini na kutokuwepo kwa usalama wa chakula. Machafuko na unyanyapaa dhidi ya wanawake na wasichana ni masuala ya kawaida nchini humo, kutokana na kutokuwepo kwa usawa wa kijinsia na tamaduni mbaya. Asilimia 42 ya wanawake wa Malawi wanaolewa katika umri wa miaka 18 na asilimia 9 katika umri wa miaka 15.

Ingawa bunge la Malawi lilipiga kura ya kubadilisha kifungu cha katiba kilichobatilisha ndoa kabla ya kufikisha miaka 18 mnamo mwaka 2017, na kulingana na shirika hilo maafisa wa Malawi sasa watatakiwa kuchukua hatua za kubadilisha vitendo vya kibaguzi miongoni mwao na jamii ili kuhakikisha kwamba sheria hiyo inatekelezeka.

Mavhinga amesema rais Chakwera atalazimika kuangazia namna ya kuboresha maisha ya watu nchini humo ambao walitengwa na walikabiliwa na unyanyasaji. Tangu mwaka 2014, kiasi visa 150 vya uhalifu viliripotiwa dhidi ya watu wenye ualbino, ikiwa ni Pamoja na mauaji, utekaji na vitisho.

Chanzo: HRW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW