1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiLibya

Shirika la Hilali Nyekundu: Waliokufa Libya wafikia 11,300

Sylvia Mwehozi
15 Septemba 2023

Vikosi vya dharura vinaendelea na zoezi la kuwatafuta maelfu ya watu ambao bado hawajapatikana kutokana na mafuriko makubwa yaliyoukumba mji wa bandari wa Derna nchini Libya.

Libyen | Flutkatastrophe Küstenstadt Darna
Picha: Ahmed Elumami/REUTERS

Wakati juhudi hizo zikiendelea, Shirika la Hilali Nyekundu la Libya limesema idadi ya vifo katika mji huo imeongezeka na kufikia watu 11,300.

soma pia: Mafuriko Libya: Idadi ya vifo huenda ikafikia 20,000

Katibu mkuu wa shirika hilo Marie el-Drese, amelieleza shirika la habari la The Associated Press kwa njia ya simu kwamba watu zaidi 10,000 hawajulikani walipo katika mji huo wa pwani wa  Mediterenia.

Mamlaka za afya hapo awali zilirekodi idadi ya vifo huko Derna kuwa ni 5,500. Mkasa huo pia umesababisha vifo vya watu 170 mahali pengine nchini Libya.

Wakati huo huo waziri wa afya wa serikali ya Mashariki ya Libya Othman Abduljaleel amesema wameanza zoezi la kuzika miili ya watu iliyopatikana katika mji wa Derna. Ameongeza kuwa miili mingi imezikwa kwenye makaburi ya pamoja nje ya mjio huo wakati mingine ikipelekwa katika miji na majiji ya karibu.

Uharibifu wa kimbunga DanielPicha: AFP/Getty Images

Juhudi za kuisaidia Libya: Juhudi za kuisaidia Libya zashika kasi

Ofisi ya uratibu wa masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa OCHA, imesema maelfu ya watu wanahitaji msaada wa dharura kufuatia mkasa huo na kutoa wito wa kupatikana dola milioni 71.4 ili kuwasaidia waathirika.

OCHA imesema msaada huo wa haraka ni katika kuwashughulikia "watu 250,000 kati ya watu 884,000 wanaokadiriwa kuwa na mahitaji katika kipindi cha miezi mitatu ijayo."

Shirika hilo limesema kuwa karibu watu 900,000 kati ya majimbo matano "wanaishi katika maeneo ambayo yameathirika moja kwa moja na kimbunga na mafuriko nchini Libya na kuathirika kwa viwango tofauti."

Kimbunga kikali kilochopewa jina la Danielkilipiga Libya siku ya Jumapili na kusababisha mafuriko mashariki mwa Libya lakini mji uliotikiswa zaidi ni wa Derna.