Shirika la HRW lasema uchaguzi wa Uganda ulikumbwa na vurugu
21 Januari 2021Shirika hilo limeongeza kusema kuwa visa vya mauaji, kukamatwa na kupigwa kwa wafuasi wa upinzani vilishuhudiwa. Wakati huohuo mawakili wa mwanasiasa Bobi Wine wanawasilisha shauri la kutaka mwanasiasa huyo kuondolewa zuio la kutotoka nyumbani kwake.
Ukiukwaji huo ni pamoja na mauaji yaliyofanywa na vikosi vya usalama, kukamatwa na kupigwa wafuasi wa upinzani, waandishi wa habari, kuingilia mikutano ya wapinzani sambamba na kufungwa kwa huduma ya intaneti. Human Rights Watch imezitaka mamlaka za Uganda kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na kuwashitaki waliohusika na ukandamizaji huo.
Tangu kampeni za uchaguzi zilipoanza mwezi Novemba mwaka 2020, vikosi vya usalama viliwaandama wanachama wa upinzani na waandishi wa habari kwa kukamata idadi kubwa ya watu wakiwemo wagombea wa urais Patrick Amuriat wa chama cha Forum for Democratic change na Robert Kyagulanyi wa National Unity Platform NUP. Novemba 18 na 19 maafisa wa usalama walikabiliana na waandamanaji waliokuwa wakidai kuachiwa kwa Bobi Wine na kusababisha watu 54 kuuwawa.
Oryem Nyeko ambaye ni mtafiti upande wa afrika katika shirika hilo amesema "uwanja wa demokrasia na uchaguzi huru na wa haki ulikuwa wa kutia mashaka katika uchaguzi huu". Aidha afisa huyo ameongeza kwamba badala ya kuzuia uhuru wa kujieleza, kutembea na kukusanyika, serikali ya Uganda inapaswa kuchukua hatua madhubuti kuboresha haki za binadamu kwa kila mtu na kuondoa vizuizi vyote vilivyobaki.
Siku mbili kabla ya uchaguzi, mamlaka ya mawasiliano ya Uganda iliamuru mitandao ya kijamii kufungwa na siku iliyofuata serikali ilizima huduma ya intaneti kote nchini humo. Mara baada ya tume ya uchaguzi kumtangaza rais Yoweri Museveni kuwa mshindi katika uchaguzi huo, maafisa wa usalama waliizingira nyumba ya Bobi Wine na tangu wakati huo hakuna mtu anayeruhusiwa kutoka na kuingia. Vikosi vya usalama pia vilimzuia mwanasiasa huyo kuelekea katika ofisi za chama chake kwa madai kubwa "ni kujaribu kuzuia mipango yoyote ya kufanya maandamano makubwa.
Vikosi vya usalama pia vimezuia watu wanaojaribu kumtembelea Kyagulanyi akiwemo balozi wa Marekani nchini humo Natalie E. Brown. Vyombo vya habari vimeripoti kwamba wanajeshi walimpiga Francis Zaake, mbunge wa upinzani alipojaribu kumtembelea Bobi Wine.
Shirika la Human Rights Watch linazitaka mamlaka za Uganda kukomesha mara moja kila aina ya unyanyasaji na vitisho kwa waandishi wa habari, wafuasi wa upinzani na viongozi akiwemo Robert Kyagulanyi. Shirika hilo limeongeza kuwa badala yake, mamlaka zina jukumu la kulinda haki, ikiwemo uhuru wa kutembea na kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa.
Vikosi vya usalama vya Uganda vinapaswa kufuata kanuni za msingi za Umoja wa Mataifa za matumizi ya silaha ambazo zinawataka maafisa wa usalama kutekeleza sheria kwa kutumia njia sizizo za vurugu na kutumia nguvu tu pale isipoepukika kulinda maisha.
Kanuni hizo pia zinahitaji serikali kuhakikisha kuwa matumizi holela au ukandamizaji na matumizi ya silaha unaofanywa na maafisa wa usalama wanaadhibiwa kwa makosa ya jinai kwa mujibu wa sheria za nchi. Human Rights Watch imeeleza kwamba ukandamizaji uliofanywa na vikosi vya usalama umedhoofisha uhalali wa uchaguzi huo.
(HRW)