Shirika la IAEA latoa ripoti kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran
19 Februari 2010Marekani imeelezea wasiwasi mpya kuhusu mpango ya nyuklia wa Iran kufuatia kutolewa kwa ripoti ya shirika la kimataifa la kuzuia usambazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, iliyopendekeza kwamba Iran huenda inaendelea na juhudi zake za kutengeneza kombora la nyuklia.
Robert Gibbs, msemaji wa rais wa Marekani Barack Obama, amesema ripoti ya sasa ya shirika la kimataifa la kuzuia utapakazaji wa silaha za nyuklia, IAEA, inaendelea kudhihirisha kushindwa kwa serikali ya Iran kuheshimu ahadi zake kwa jumuiya ya kimataifa na kutimiza wajibu wake. Gibbs amesema Marekani bado inashikilia msimamo wake wa kuichukulia hatua kali Iran iwapo itashindwa kutimiza majukumu yake na kuachana na mpango wake wa nyuklia.
Marekani tayari inaongoza juhudi za kulitaka baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liiwekee Iran awamu ya nne ya vikwazo kwa sababu ya mpango wake wa nyuklia. Urusi ambayo mpaka sasa imekuwa ikisita kupanua vikwazo dhidi ya Iran inaiunga mkono Marekani.
Shirika la IAEA limesema katika ripoti yake kwamba Iran huenda inatengeneza kombora la nyuklia na imeanza kurutubisha uranium kwa kiwango cha juu.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani, Philip McCrowley, amewaambia waandishi wa habari kwamba wasiwasi unazidi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran lakini hawezi kufafanua kwa nini nchi hiyo inakataa kukaa kwenye meza ya mazungumzo ili kujibu maswali ambayo yamejitokeza. Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani Bi Hilary Clinton ameitaka Iran ifikirie upya sera zake hatari.
Ripoti ya kurasa kumi iliyotolewa na shirika la kimataifa la IAEA na ambayo itajadiliwa kwa kina na magavana wa shirika hilo mwezi ujao, pia imethibitisha kwamba urutubishaji wa uranium kwa kiwango cha juu kimsingi unaipa uwezo Iran kukaribia kiwango cha kutengeneza bomu la nyuklia.
Lakini afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Marekani amesema ripoti hiyo pia imeonyesha wazi kuwa Iran inarutubisha uranium katika kiwango ambacho kitaifanya ichukue miaka mingi kuweza kutengeneza bomu la nyuklia. Afisa huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe ameongeza kuwa matokeo ya uchunguzi wa shirika la IAEA yamedhihirisha kuwepo matatizo ya kiufundi yanayoutatiza mpango wa nyuklia wa Iran. Mashine za kurutubisha uraniun zinakwama na madini ya uraniun huenda yanakaribia kuisha.
Ripoti ya shirika la IAEA imeeleza bayana mwenendo wa Iran kutoshirikiana na shirika hilo. Iran imeshawahi kurutubisha uranium kwa viwango vya chini visivyozidi asilimia tano katika kinu chake cha nyuklia cha Natanz, huku ikikaidi amri ya Umoja wa Mataifa ikome kufanya hivyo na pia bila kujali tayari inakabiliwa na awamu ya tatu ya vikwazo vya umoja huo.
Ripoti ya shirika la IAEA ni ya kwanza chini ya uongozi wa mkurugenzi mpya wa shirika hilo, jenerali Yukiya Amano ambaye anaonekana akichukua mwelekeo wa kukabiliana na Iran akilinganishwa na mkurugenzi wa shirika la IAEA aliyeondoka, Mohammed El Baradei.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/RTRE
Mhariri: Othman Miraji