Vurugu zatatiza kuagwa mwili wa Raila Odinga
17 Oktoba 2025
Baada ya kutwa nzima ya mshikemshike na pilka pilka,shughuli ya kutoa heshima za mwisho kwa marehemu waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga imefanyika. Familia ya marehemu akiwemo mjane Mama Idah Odinga na viongozi wakuu serikalini ndio walikuwa wa kwanza kuiona maiti ya hayati kigogo Raila Odinga.
Kofia yake iliyokuwa kitambulisho chake rasmi ilipachikwajuu ya jeneza lililokuwa wazi. Maiti ilifunikwa pia kwa kitambaa cha njano ambayo ndiyo rangi rasmi ya chama chake cha siasa cha ODM.
Shughuli ya kutoa heshima za mwisho kwa hayati waziri mkuu wa zamani Raila Odinga ilihamishiwa uwanja wa michezo wa kimataifa wa Kasarani baada ya vurugu kuzuka kwasababu ya umati mkubwa uliojitokeza kushiriki.Mamia kwa maelfu walijitokeza kwenye uga huo wa kimataifa na baada ya muda hali ikawa ya mshikemshike.
Idadi kubwa ya wafuasi wa Odinga yapelekea shughuli kuhamishwa
Polisi walilazimika kufyatua risasi hewani ili kuwatawanya waombolezaji waliokuwa wanawashinda nguvu maafisa wa usalama waliokuwa wanapiga doria.
Mwendo wa adhuhuri hali ilikuwa si hali nje ya majengo ya bunge ambako wafuasi wa mwendazake, kigogo Raila Odinga walikusanyika kwa wingi. Yaliyojiri yalimsukuma spika wa bunge la taifa Moses Wetangula kuihamisha shughuli hiyo hadi uga wa Kasarani.
Kiranja wa bunge Sylvanus Osoro aliafiki kuwa idadi ya waliotokeza ilizua changamoto.
Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga alikiri kuwa waombolezaji wana simanzi ila ni muhimu amani idumishwe.
Malefu ya wafuasi walimiminika kwenye uwanja wa majengo ya Bunge na kupanda langoni na kwenye kila sehemu iliyokuwa na viambaza.
Juhudi za wabunge na viongozi wengine serikali kuwazuwia vijana hao ziliambulia patupu ila lilitolewa tangazo kuwa hafla imehamishwa. Wakenya waliojitokeza walikuwa na haya ya kusema kuhusu matukio ya leo.
Kutwa nzima wafuasi wa hayati Raila Odinga waliandamana guu mosi guu pili na msafara wa maiti yake kutokea uwanja wa kimataifa wa ndege wa JKIA hadi uwanja wa michezo wa Kasarani wakiimba na kupiga mayowe.
Usalama waimarishwa kwenye makaazi ya Raila
Katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee, mipango ilibadilika ghafla na wataalam wa kuandaa maiti walilazimika kuelekea uwanja wa michezo wa Kasarani kuisubiri.
Kwa sasa usalama umeimarishwa katika makaazi ya Bondo na Nairobi ya hayati Raila Odinga ili kuipa nafasi mipango ya maziko kutimia kwa amani ukizingatia matukio ya leo.
Duru zinaeleza kuwa polisi wameweka vizuizi kwenye barabara inayoelekea kwake nyumbani mtaani Karen.Kulingana na ratiba rasmi, kigogo huyo atapokea heshima kamili kama alivyoamuru Rais William Ruto.
Kwa mujibu wa wosia wake, hayati Raila Odinga alipendelea kuzikwa katika kipindi cha saa 72 baada ya kifo.