1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shughuli za kiuchumi zaanza kurejea nchini Uganda

Lubega Emmanuel22 Julai 2020

Rais Museveni wa Uganda amelegeza baadhi ya hatua za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 zilizotangazwa tangu mwezi Machi. Museveni ameruhusu kufunguliwa tena maduka makubwa, saluni na usafiri wa bodaboda.

Uganda Kampala | Coronavirus | Straßenverkäufer
Picha: Getty Images/AFP/B. Katumba

Baada ya kipindi cha miezi minne cha kufungwa kwa biashara nyingi katika kitovu cha mji wa Kampala, rais Museveni amelegeza kanuni hizo kwa kile alichokariri kuwa kwa ushauri wa wanasayansi. Majengo 110 ya maduka yameruhusiwa kufunguliwa lakini kwa masharti makali ya kuhakikisha kuwa wafanyabiashara wanaepusha maambukizi ya virusi vya Corona.

Miongoni mwa masharti hayo ni kuhakikisha kuwa mteja ana barakoa, anapimwa kiwango chake cha joto na pia jina na anwani yake kusajiliwa. Akihutubia taifa usiku wa kuamkia Jumatano, Museveni aidha amefupisha muda wa kutotoka nje kwa saa mbili. Kipindi hicho sasa kitaanza saa tatu usiku.

Tangazo la kulegeza kanuni lilisubiriwa kwa shauku kubwa hususan na waendeshaji pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda wakitarajia kuwa wataruhusiwa kubeba abiria. Lakini rais Museveni amewapa masharti makali ambayo watatakiwa kuhakikisha wanatimiza ili waanze kazi tarehe 27 mwezi huu. Miongoni mwa masharti hayo vilevile ni kuwa na kipima joto na kutakatisha pikipiki kabla ya kumsafirisha abiria.

Mfanyakazi wa shirika la msalaba mwekundu akipima joto la mwananchi kabla ya kuingia soko la Nakasero.Picha: AFP/S. Sadurni

Huku akielezea kuwahurumia zaidi ya walimu laki tatu na nusu wa shule na taasisi binafsi za elimu ambao waajiri wao walisitisha kuwalipa mishahara tangu mwezi Machi, rais Museveni amefafanua kuwa bado wana mjadala mzito kuhusu suala la kufungua tena shule na taasisi za elimu. Walimu,wazazi na wanafunzi watasubiri kwa mwezi mmoja zaidi kufahamu kama masomo yatanza tena.

Katika hatua ya kuendelea kudhibiti maambukizi kutoka nje ya nchi, mipaka ya Uganda itabaki imefungwa na pia safari za ndege za abiria zingali marufuku katika kipindi hiki.

Hadi sasa hakuna kifo kimetangazwa rasmi kutokana na COVID-19 na idadi ya watu waliogunduliwa kuwa na ugonjwa huo ni 1,072. Idadi hii haijumulishi raia wa kigeni ikiwemo madereva wa malori ya mizigo waliorudishwa katika nchi zao baada ya kugunduliwa kuwa na virusi vya Corona. Mbinu hii imepingwa na shirika la afya duniani WHO likisisitiza kuwa mgonjwa aorodheshwe katika nchi alikogunduliwa kuwa na virusi vya Corona.

Lubega Emmanuel DW Kampala.