Shughuli za serikali ya Marekani zakwama
20 Januari 2018Kiongozi wa wabunge wa Republican walio wengi bungeni, Seneta Mitch McConnel, amesema baraza la seneti linaweza kukutana tena leo. ''Ni matumaini yangu muafaka utapatikana,'' alisema McConnel jana usiku, baada ya baraza hilo kushindwa kupitisha mswada wa kurefusha ufadhili wa matumizi ya serikali. Mswada huo ulihitaji kura 60 katika baraza la Seneti lenye wanachama 100, lakini ukaungwa mkono na maseneta 50 pekee.
Hatua hiyo inakwamisha masuala ya bajeti ambayo yangesaidia kuwalipa wafanyakazi wa shirikisho pamoja na mashirika kadhaa yasiyo na majukumu muhimu kwa siku 30. Kama sehemu ya kuipigania bajeti hiyo, wabunge wa upinzani wa chama cha Democratic wanataka sheria kuzuia kurejeshwa kwenye nchi zao, vijana wahamiaji ambao waliingia Marekani kinyume cha sheria wakati wakiwa watoto.
Wademocrat wamekataa kuunga mkono mpango huo wa dakika ya mwisho kutoka na kile walichokiita azimio la matumizi bila ya kufikiwa kwa makubaliano kuhusu sera ya uhamiaji. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani, viongozi wa Republican wanatafuta njia mpya za kukutana tena leo ili kufikia makubaliano na wademocrat kwa lengo la kurefusha ufadhili wa shughuli za serikali hadi Februari 8.
Trump atimiza mwaka mmoja madarakani
Hao yanajiri wakati ambapo Rais Donald Trump anaadhimisha mwaka mmoja tangu alipoingia madarakani Januari 20, 2017. Trump ambaye ameahirisha safari yake kwenye Mar-a-Lago, Florida, amewalaumu wabunge wa Democratic kutokana na hatua hiyo, kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.
''Wademocrats wanazingatia zaidi siasai kuhusu wahamiaji walioingia nchini kinyume cha sheria, kuliko jeshi letu au usalama katika eneo hatari la mpaka wa kusini. Wangeweza kufikia makubaliano, lakini wameamua kuwateka Wamarekani kutokana na madai yao,'' alisema Trump.
Hata hivyo, Ikulu ya Marekani imesema haitofanya mazungumzo yoyote yale na Wademocrat kuhusu uhamiaji, hadi hapo mkwamo huo utakapomalizika. ''Hatutojadiliana kuhusu hadhi ya wahamiaji wanaovunja sheria, huku Wademocrats wakiwashikilia mateka wananchi wetu wanaofuata sheria kuhusu madai yao yasio na msingi,'' alisema msemaji wa Ikulu, Sarah Huckabee Sanders.
Hali hii sasa inamaanisha kwamba mashirika kadhaa ya serikali ya Marekani hayataweza kuendelea na shughuli zake na maelfu ya wafanyakazi wasio na majukumu muhimu sana watalazimishwa kwenda likizo ya bila malipo. Wademocrat wengi walipinga mswada huo kwa sababu juhudi zao za kujumuisha hatua za ulinzi wa mamia ya maelfu ya wahamiaji wengi wao vijana, zilipingwa na Rais Trump na viongozi wa Republican.
Haijajulikana shughuli za serikali ya Marekani zitakwama kwa muda gani. Mkwamo wa shughuli za serikali Marekani ulitokea mwaka 2013, na ulidumu kwa siku 16. Kabla ya kufanyika kwa kura hiyo jana usiku, Mkurugenzi wa bajeti wa Ikulu ya Marekani, Mick Mulvaney amewaambia waandishi habari kwamba kuna uwezekano wa kufikiwa kwa muafaka, kabla ya ofisi za serikali hazijafunguliwa tena siku ya Jumatatu.
Hata hivyo, shughuli za shirikisho na operesheni zozote za kijeshi ambazo zinazingatiwa kuwa muhimu zitaendelea, lakini maelfu ya wafanyakazi wa serikali wanatarajiwa kupatiwa fursa, iwapo makubaliano hayatofikiwa kabla ya Jumatatu.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AFP, Reuters, DW http://bit.ly/2rpdzjB
Mhariri: Bruce Amani