1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shule zimefunguliwa Ujerumani lakini kwa uvaaji wa barakoa

13 Agosti 2020

Ujerumani imefungua tena milango ya shule kwa maelfu ya wanafunzi baada ya mapumziko ya msimu wa kiangazi na baada ya miezi kadhaa ya wanafunzi kusoma wakiwa nyumbani kutokana na janga la virusi vya corona.

Deutschland | Coronavirus | Schulstart
Picha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Ujerumani imefungua tena milango ya shule kwa maelfu ya wanafunzi baada ya mapumziko ya msimu wa kiangazi na baada ya miezi kadhaa ya wanafunzi kusoma wakiwa nyumbani kutokana na janga la virusi vya corona. Lakini ni wazi hali haitokuwa kama muhula wa kawaida.

Mwaka mpya wa masomo umeanza nchini Ujerumani baada ya miezi kadhaa ya wanafunzi kusoma wakiwa nyumbani kutokana na kadhia ya virusi vya corona. Jimbo lenye idadi kubwa ya watu nchini Ujerumani la North Rhine-Westphalia limefungua tena milango kwa maelfu ya wanafunzi, lakini kwa tahadhari na limetangaza orodha ya hatua chungunzima za kukabiliana na kusambaa virusi vya corona.

Ulazima wa kuvaa barakoa katika maeneo ya shule

Barakoa mkononi mwa mwanafunzi darasani mjini BerlinPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Katika jimbo hilo wanafunzi wote watalazimika kuvaa barakoa pindi wakiwa kwenye viunga vya shule na hata darasani. Kulingana na maafisa wa jimbo hilo hatua hizo mpya zinalenga kuwaruhusu wanafunzi kuanza muhula mpya wa masomo wakiwa salama katika wakati ambao Ujerumani inashuhudia ongezeko linalotia wasiwasi la maambukizi ya virusi vya corona.

Katika shule ya sekondari ya Friedrich-Ebert iliyopo mjini Bonn, mwalimu wa hesabu na michezo Stephan Grothe ameiambia DW kuwa anahisi furaha kwamba masomo yamerejea na kanuni ya kuvaa barakoa ni muhimu kwa kuwa kitisho cha COVID-19 bado haijaondoka."Nadhani inaeleweka na ni muhimu hata kama itakulazimu kuizoea hali hiyo. Hakuna anayetaka shule zifungwe baada ya wiki mbili au tatu.'' alisema Grothe.

Soma zaidi:Matumaini ya chanjo ya virusi vya corona Ujerumani yaongezeka

Nchini Ujerumani kanuni za afya zinazowekwa kupambana na kusambaa virusi vya corona ikiwemo mashuleni zinatofautiana kutoka jimbo moja hadi jingine. Hadi sasa ni jimbo la North Rhine-Westphalia pekee miongoni mwa majimbo 16 ya Ujerumani ndiyo limetangaza sharti la kuvaa barakoa kwa wanafunzi. Na kwa hakika siyo wanafunzi wote waliopokea uamuzi huo kwa furaha, kama anavyofafanua zaidi mwanafunzi Corine Santara."Ninaishi Rhineland-Palatinate, lakini ninasoma jimboni North Rhine-Westfalia. Huko Rhineland-Palatinate hakuna sharti la kuvaa barakoa darasani, lakini hapa kuna sharti hilo na ninadhani kwa kiasi fulani siyo haki.''

Hayo yanajiri wakati Waziri wa Afya wa Aerikali Kuu ya Ujerumani, Jens Spahn amesema leo kuwa ana matumaini kwamba nchi hiyo itapata chanjo dhidi ya virusi vya corona katika muda wa miezi michache inayokuja au mwaka ujao. Ingawa Spahn amejizuia kutaja tarehe rasmi ya kupatikana chanjo hiyo, lakini amesisitiza kuna ishara zote kuwa itapatikana haraka na kazi kubwa inaendelea kulifanikisha jambo hilo.

Chanzo: DW