Siasa kali za kizalendo zinaathiri vita dhidi ya rushwa
25 Januari 2017Katika ripoti yake ya kila mwaka kuhusu rushwa duniani, ambayo huziorodhesha nchi kulingana na kiwango chake cha rushwa katika sekta ya umma, Transparency International limesema siasa kali za uzalendo za mrengo wa kulia ni dawa isiyofaa.
Mwenyekiti wa TI Jose Ugaz amesema katika nchi zenye viongozi wa siasa za kizalendo au za kimabavu, viwango vya demokrasia hupungua na kushuhudiwa muundo wa majaribio ya kuyakandamiza mashirika ya kiraia, kupunguza uhuru wa habari na kudhoofisha uhuru wa idara ya mahakama. Ugaz amesema katika taarifa kuwa viongozi hao badala ya kuukabili ubepari, wanaweka mifumo mibaya hata zaidi ya ufisadi
Wasiwasi pia unaongezeka kuhusu Marekani ambapo Trump aliingia madarakani wiki iliyopita kufuatia kampeni iliyowakemea wanasiasa matajiri na akaahidi kuondoa rushwa serikalini. Lakini Finn Heinrich, mkurugenzi wa utafiti katika shirika hilo la TI amesema hana matumaini kama bilionea huyo wa Marekani ataweza kutimiza ahadi zake ikizingatiwa kuwa anakabiliwa na mgongano wa maslahi ya kibiashara, mashambulizi yake kwenye vyombo vya habari, na kukataa kwake kutoa marejesho ya matumizi ya mwaka. "Trump alisema ataukabili ufisadi lakini ukiangalia vitendo vyake kufikia sasa kuna upendeleo, mkwe wake wa kiume ni mshauri mkuu, watu katika baraza lake la mawaziri wana mgongano wa maslahi. Sio watu wanaosimamia uwazi. Ni watu wanaosimamia mipango ya siri, mipando ya rushwa. Hivyo tuna wasiwasi mkubwa kuwa hataweza kufanya alichoahidi na badala yake atafanya mambo kuwa mabaya zaidi"
Mawakili wa masuala ya Katiba na maadili waliwasilisha mahakamani kesi wakidai kuwa Trump amegubikwa na mgongano wa maslahi. Trump alipuuzia madai hayo akisema kesi hiyo haina msingi. Ripoti ya mwaka huu iliziorodhesha nchi 176 kwa mizani ya pointi 0 hadi 100, ambapo sifuri inamaanisha nchi hiyo inakabiliwa na ufisadi zaidi na 100 inaashiria ni nchi isiyo na tatizo la ufisadi.
Na Marekani imeshuka nafasi mbili hadi 18 katika orodha ya sasa ya viwango vya rushwa, ikiwa na pointi 74 hadi 100 kutoka 76 katika mwaka wa 2016. Data za ripoti hiyo zinazingatia tafiti kutoka Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika, shirika la utafiti la kimataifa la Uingereza Economist Itelligence unit na mashirika mengine.
New Zealand na Denmark kwa pamoja zilichukua nafasi ya kwanza kwa kupata pointi 90, huku Finland, Sweden, Uswisi na Norway zikikamilisha orodha ya tano bora ya nchi zisizokuwa na kiwango kikubwa cha ufisadi. Somalia ndiyo iliyoshika mkia kwa mwaka wa kumi mfululizo, ikifuatwa na Sudan Kusini, Korea Kaskazini na Syria.
Qatar ilionyesha kiwango kikubwa cha kushuka imani katika mwaka wa 2016 baada ya kashfa iliyohusisha shirikisho la kandanda duniani FIFA na ripoti za ukiukaji wa haki za binaadamu.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Yusra Buwayhid