1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Siasa ni kazi ambayo inamuumiza binadamu"

Maja Dreyer11 Aprili 2006

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wanazingatia masuala mawili ya kisiasa yaliyogonga vichwa vya habari hapo jana, yaani kwanza kujiuzulu mwenyekiti wa chama cha SPD nchini Ujerumani na pili rais wa Ufaransa kufuta kabisa sheria ya ajira iliyopingwa sana katika maadamano na migomo nchini humo.

Kwa kweli, matokeo ya kisiasa ya wiki hii hapa nchini Ujerumani yalianza na habari moto moto. Miezi mitano tu baada ya kuchukua wadifha wake, mwenyekiti wa chama cha Social Democrats, SPD, Matthias Platzeck, alijiuzulu kutokana na afya yake mbaya. Mhariri wa gazeti la “Westfälische Rundschau” la mjini Dortmund ana maoni yafuatayo kuhusu uamuzi huo:
“Bw. Platzeck alijulikana kama mtu anayeweza kuaminika. Na hiyo inaonekana pia katika uamuzi wake wa kujiuzulu. Platzeck alisema cheo hicho kilizishinda nguvu zake. Kusema haya ni hatari kubwa katika dunia ya leo ambapo watu dhaifu wanaangaliwa kwa jicho baya. Siasa ni kazi ambayo inamuumiza binadamu. Platzeck alikubali jambo hilo na Platzeck akajiuzulu. Kwa sababu hiyo anapaswa kuheshimiwa.”

Gazeti la “Frankfurter Rundschau” linatathmini kwamba kujiuzulu kwa Platzeck kunakiharibia chama cha SPD. Tunasoma:
“Faida ya Platzeck ilikuwa kwamba aliaminika. Baada ya siasa ya kuwa na uchu wa mamlaka ya kansela wa zamani Gerhard Schröder na mwenyekiti wa zamani Franz Müntefering, chama cha SPD kwa mara ya kwanza, baada muda mrefu, kilianza kujiangalia. Baada ya Platzeck kuondoka haijulikani ikiwa chama cha SPA kitaweza tena kuwavutia watu wengi na vile vile ikiwa kitaweza kutafuta malengo yake maalum wakati kinapotawala pamoja na chama cha Christian Democrats ndani ya serikali ya mseto.”

Aliyeteuliwa kuwa mrithi wa Bw. Platzeck katika kukiongoza chama cha SPD ni Kurt Beck, waziri mkuu wa mkoa wa Rhineland-Palatine. Kulingana na mhariri wa gazeti la “Thüringer Allgemeine” la mjini Erfurt, Bw. Beck ana nguvu za kutosha kupambana na Kansela Angela Merkel. Gazeti limeandika:
“Sasa ni Kurt Beck badala ya Matthias Platzeck. Hivyo chama cha SPD kinarudi katika asili yake. Hii, bila shaka, ni hatua nzuri kwa sababu lazima chama hicho kionyeshe sifa nzuri badala ya kuendelea na urafiki wake na chama cha CDU. Kurt Beck anafaa kwa kazi hiyo kwa kuwa wapiga kura wanapenda namna yake ya kutatua matatizo. Hata katika wakati ngumu kwa chama chake, Beck aliweza kushinda katika uchaguzi wa mkoa wake.”

Na kutoka hapo tunaelekea Ufaransa, ambapo baada ya maandamo makubwa yaliyoendelea kwa wiki nyingi, Rais Jacques Chirac jana aliarifu kwamba sheria mpya ya ajira itafutwa. Gazeti la “Schwäbische Zeitung” limeandika:
“Baada ya wiki 11 ya mzozo wa kijamii, hakuna hata mtu mmoja aliyeshinda nchini Ufaransa. Wanasiasa walishindwa kwa kuwa wameharibu zaidi sifa yao. Wanaharakati wa jumuiya za wafanyakazi walishindwa kwa sababu, kwa mara nyingine, wameonyesha hawayakubali mabadiliko yoyote. Na vijana ambao hawana ajira sasa wanategemea msaada wa kiserikali. Ni majivu tu yaliyobakia.”

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW