1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za Ujerumani: Uchaguzi wa mapema wanukia

11 Novemba 2024

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema yuko tayari kuitisha kura ya imani juu yake katika mwaka huu wa 2024 iwapo pande zote zitaridhia ili kupisha uchaguzi wa mapema. Amesema yuko tayari kura hiyo ifanyike haraka

ARD-Sendung «Caren Miosga» mit Bundeskanzler Scholz
Picha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Kansela Scholz ambaye hapo awali baada ya kuvunjika serikali yake ya muungano wa vyama vitatu alitangaza kuwa hatua hiyo ingefanyika katikati ya mwezi Januari mwakani ambapo chini ya sheria za uchaguzi za Ujerumani ingewezekana uchaguzi kufanyika mwishoni mwa mwezi Machi mwaka ujao lakni sasa Kansela wa Ujerumani amesema yuko tayari kuitisha kura hiyo ya imani ili kuwezesha uchaguzi wa mapema kufanyika.

Scholz pia amekanusha madai kwamba yeye ndiye alisababisha kuvunjika kwa muungano wa vyama vitatu makusudi. Serikali yake ya muungano ilisambaratika Jumatano iliyopita.

Soma Pia: Scholz atoa rai ya utulivu kumaliza mzozo wa kisiasa 

Kansela wa Ujerumani amesema ikiwa pande zote zitaridhia, kura hiyo inaweza kuitishwa mwaka huu lakini amesisitiza kwamba kuna mambo mengi ambayo yanapaswa kuzingatiwa.

Kansela wa Ujerumani katika mahojiano na Televisheni ya Ujerumani, ARDPicha: Carsten Koall/dpa/picture alliance

Alipoulizwa kuhusu kura hiyo ya kuwa na Imani naye kama inaweza kufanyika mnamo mwezi Desemba kabla ya Krismasi Scholz alisema: ‘'Naunga mkono kwa dhati hili lifanyike, kwa sababu pia nataka lifanyike haraka. Sitaki kupewa mamlaka mapya kutoka kwa mtu mwingine yeyote, bali nataka niidhinishwe na wananchi kupitia kura zao nyingi watakazopiga kukichagua chama changu cha SPD.''

Wakati huo huo, maafisa wa uchaguzi wa Ujerumani katika ngazi ya shirikisho na majimbo wanapanga kukutana leo Jumatatu kujadili maandalizi ya uchaguzi wa mapema wa Bunge.

Mkutano huo wa mtandaoni utafanyika saa chache kuanzia sasa pia unatarajiwa kuangalia taratibu mpya kufuatia mabadiliko katika kanuni za uchaguzi.

Kamishna wa uchaguzi asemaje?

Kamishna wa Uchaguzi wa kitaifa Ruth Brand, amesema tayari ameanza maandalizi ya uchaguzi huo mpya ili kukabiliana na changamoto zinazotokana na muda mfupi uliopo iwapo itatangazwa kuwa Ujerumani itafanya uchaguzi mpya. 

Katika barua kwa Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz kamishna huyo pia ametahadharisha kuhusu "hatari zilizojificha" kwa sababu ya muda kuwa mfupi na changamoto za vifaa.

Kamishna wa Uchaguzi wa kitaifa cnhini Ujerumani Ruth BrandPicha: Jens Krick/Flashpic/picture alliance

Soma Pia: Upinzani Ujerumani wataka kura ya imani na serikali 

Kamishna Brand, amesema anakusudia kutumia kikamilifu kipindi cha siku 60 kilichowekwa kikatiba kati ya kuvunjwa kwa bunge na kufanyika uchaguzi mpya ili kuhakikisha kuwa hatua zote muhimu zinachukuliwa kwa kufuata sheria na pia kwa wakati.

Hata hivyo upinzani nchini Ujerumani umeyakosoa matamshi ya Ruth Brand, ukisema yanaweza kuwa yanaingilia kati upangaji wa tarehe ya uchaguzi.

Vyanzo: DPA/AFP