1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za Zimbabwe

Munira Muhammad/Reuters12 Machi 2009

Mahakama kuu nchini Zimbabwe imeamuachillia kwa dhamana Roy Bennet afisa wa ngazi za juu wa chama cha Movement for Democratic Change.

Afisa wa MDC Roy BennettPicha: AP


Kuachiliwa kwa Bennett, sahiba mkuu wa kiongozi wa MDC ambaye pia ni waziri mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangira, baada ya mwezi mzima gerezani, huenda kukazima mvutano katika serikali ya muungano baina ya Tsvangirai na Rais Robet Mugabe.Wakati huo huo, Australia inakuwa nchi ya kwanza ya Magharibi kuahidi kuisadia kifedha Zimbwabwe.



Pale Rais Robert Mugabe na Waziri mkuu Morgan Tsvangirai walipotia saini makubaliano ya kubuni serikali ya muungano- Roy Bennett aliteuliwa kuwa waziri mdogo wa kilimo. Baraza la mawaziri lilipoapishwa Bennett hakuwepo- kwani tarehe 13 Februari alikamatwa na polisi na kushtakiwa kwa mashtaka ya ugaidi.


Kukamatwa kwake nusura kusambaratishe serikali ya muungano kati ya MDC na ZANU PF. Wiki iliopita mahakama nchini Zimbabwe ikaamuru Bennett aachiliwe kwa dhamana, lakini waendeshaji mashtaka wa serikali wakapinga uamuzi huo. Hata hivyo, jana mahakama kuu ikatoa uamuzi wake, kiongozi huyu wa MDC aachiliwe kwa dhamana ya dola elfu tano.


'' Nimewasamehe walioendeleza mateso dhidi yangu......la muhimu sasa ni kusameheana, tuvumiliane na tuwe na maelewano baina yetu wanasiasa ili tuendeleze taifa letu.'' ndio yalikuwa matamshi ya Bennett muda mfupi tu baada ya kuachiliwa .


Matamshi ya Bennett yanatia moyo, kuwa ingawa bado serikali ya kitaifa nchini Zimbabwe ina changamoto nyingi, kutokana na uhasama baina ya MDC na ZANU-PF kufuatia uchaguzi tata....pengine wanaweza wakazizika tofauti zao ili kuikomboa Zimbabwe kutoka uchumi uliodorora na utawala mbaya.


Mapema wiki Rais Robert Mugabe pia alitoa mwito wa kusameheana na kutaka Tsvangirai aungwe mkono katika jitihada zake za kuikarabati Zimbabbwe. Kuachiliwa kwa Bennet huenda pia ikawa ndio dawa ya kutibu mgogoro ndani ya serikali hii ya mwezi mmoja.


Ukosefu wa ajira umefikia aslia mia 90 nchini Zimbabwe, uhaba wa bidhaa muhimu kama vyakula , na uchumi ulioanguka ukitegemea msaada wa wafadhili wa kigeni. Nchi za magharibi zimesema bayana kwamba usaidizi wao kwa Zimbabwe utategemea jinsi ya kuwepo marekebisho ya utawala na kukomaa demokrasia. Australia, hata hivyo, imetangaza iko tayari kunyosha mkono wa usaidizi kwa Zimbabwe.


Austaralia inakuwa taifa la kwanza la Magharibi kuahidi kusaidia kifedha. Naibu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Asha Rose-Migiro amedokeza kuwa pasi na uchumi wa Zimbwabwe kupigwa jeki ya kifedha- itakuwa vigumu serikali hiyo kudumisha sheria na haki za kibinadamu.


'' Zimbabwe lazima isaidiwe ili izingatia sheria, utawala bora na haki za kibinadamu, Hii ni changamoto kwa Afrika nzima, na hawana budi kujibidiisha zaidi kuisaidia nchi hiyo ili iwajibike.....ndio matamshi ya naibu katibu huyo wa Umoja wa Mataifa, Asha Rose Migiro.


Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, naye amezihimiza dola za Magharibi kuisadia Zimbabwe ijikwamuwe kiuchumi hasa sasa wakati mataifa mengi yanaathirika na mgogoro wa kiuchumi. Kikwete ambaye hakuwa kimya kutoa shtuma dhidi ya Mugabe, baada ya uchaguzi tata nchini humo, sasa anasema Harare inajitahidi kupiga hatua baada ya kubuni serikali ya muungano, hivyo inahitaji angalau kushikwa mkono.