Sierra Leone yapiga mnada almasi ya "Amani"
5 Desemba 2017Moja kati ya almasi kubwa kabisa duniani iliuzwa kwa kitita cha dola milioni 6.8 na nchi ya Sierra Leone siku ya Jumatatu ili kugharamia miradi ya maendeleo ya nchi hiyo, na kutoa pigo kubwa kwa walanguzi wa maliasili kama hizo barani Afrika.
Almasi hiyo iliyokuwa na ukubwa wa yai la kuku , yenye karati 709 iligunduliwa na mchungaji mmoja wa kanisa na ilifikishwa katika mnada mjini New York na Laurence Graff, tajiri mkubwa bilionea Muingereza na muuzaji wa vito vya thamani , kwa mujibu wa kundi la Rapaport, mtandao wa kimataifa wa biashara ya almasi ambalo lilihusika katika biashara ya almasi hiyo.
Mapato ya mauzo ya almasi hiyo ambayo ilipewa jina "Almasi ya amani," serikali itapata asilimia 59 ya mauzo ama kiasi cha dola milioni 3.9 katika kodi ili kuweza kugharamia mradi ya maji safi, umeme, shule, vituo vya afya na barabara, amesema Martin Rapaport wa kundi hilo la Rapaport.
"Wakati serikali katika bara la Afrika , zimekuwa zikielezwa kutumbukia katika rushwa, na utajiri wa madini hauwafikii wananchi ", amesema Abdulai Bayraytay , msemaji wa rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma, katika mkutano na waandishi habari.
Mauzo hayo katika mnada yanakuwa ya kwanza kutokana na almasi iliyopatikana nchini Sierra Leone yalifanyika hadharani, na maafisa wa serikali walisema wanamatumaini itakuwa hatua ya kwanza mbele katika kumaliza biashara haramu ya almasi nchini humo.
Almasi zilichochea vita
Almasi zilichochea vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sierra Leone katika miaka ya 1990, wakati wapiganaji waasi walipowalazimisha raia kuchimba mawe hayo ya thamani na kununua silaha kutokana na mapato ya mauzo ya almasi , na kusababisha kubatizwa jina la "Almasi za damu".
Umoja wa Mataifa uliondoa marufuku iliyowekwa kwa mauzo ya almasi nje ya nchi hiyo mwaka 2003, lakini sekta hiyo ambayo ni biashara ya mabilioni ya dola bado imezungukwa na walanguzi.
Kiasi kilichobaki cha mapato ya mauzo ya almasi hiyo kitakwenda katika kundi la nchi humo linaloangalia miradi ya maendeleo, mchungaji huyo wa kanisa na wachimbaji wengine ambao waligundua almasi hiyo na kuifikisha serikalini, Rapaport alisema.
"Italeta ushawishi kwa wachimbaji wengine nchini humo," Chifu Paul Ngaba Saquee, mkuu wa wilaya ya Kono mashariki mwa Sierra Leone, ambako almasi hiyo ilipatikana mwezi Machi , aliwaambia waandisjhi habari.
"Badala ya kupitishwa katika vichochoro ambako almasi nyingi zinapatikana , watazifikisha na kuweka mezani mbele ya serikali, " alisema mjini New York . " Huenda huu utakuwa mwanzo wa siku mpya nchini Sierra Leone."
Juhudi za kwanza kuiuza almasi hiyo zilishindwa mwezi Mei wakati Sierra Leone ilipokataa kiwango cha juu cha malipo ya dola milioni 7.8.
Mara hii, jiwe hilo la thamani lilioneshwa kwa watu 70 ambao walikuwa na uwezo wa kulinunua na maombi saba yaliwasilishwa, kwa mujibu wa Rapaport.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman