Sigmar Gabriel achaguliwa upya kuiongoza SPD
15 Novemba 2013Mkutano huo mkuu wa dharura wa chama cha Social Democratic unafanyika katika wakati ambapo mazungumzo ya kuunda serikali kuu ya muungano kati ya vyama ndugu vya Christian Democratic Union,CDU, Christian Social Union, CSU na Social Democratic, SPD, yameshika kasi. Katika zoezi la upigaji kura, mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel, amejikingia asilimia 83.6 tu ya kura safari hii - Ni haba ikilinganishwa na asilimia 94.2 alizopata alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2009 au asilimia 91.8 alizojikingia miaka miwili baadaye.
Hata hivyo Sigmar Gabriel amewashukuru wajumbe mkutanoni kwa kile alichokiita "matokeo ya dhati ya uchaguzi katika wakati huu wa kipekee." Hapo alikuwa akigusia wakati huu ambapo mkutano wa kuunda serikali kuu ya muungano unaendelea huku SPD wakishinikizwa na wanachama wake wanaotaka kuona madai yao muhimu yanazingatiwa.
Hakuna Muungano bila ya madai kuzingatiwa
Ili kutuliza hofu za wanachama, mwenyekiti wa SPD, Sigmar Gabriel amesema, "Hatutofuata kwa mara ya pili mkondo wa siasa ambayo SPD kwa mara nyengine tena itakiuka muongozo wake. Ndio maana mshahara wa chini wa Euro 8.5 kwa saa kwa wote, lazima ukubaliwe, bila ya hilo hakuna muungano utakaofanyika pamoja na SPD."
Gabriel ameutaja ushirikiano pamoja na muungano wa CDU-CSU kuwa ni ushirikiano wa busara na wa muda. Anasema juhudi za kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi na kupigania uraia wa nchi mbili ni juhudi za maana zinazostahiki kupiganiwa katika mazungumzo hayo ya kuunda serikali ya muungano. Miito imehanikiza pia katika mkutano huo mkuu mjini Leipzig kutaka chama cha SPD kifanyiwe mageuzi yanayoambatana na wakati.
SPD chawachagua viongozi wake
Baadaye hii leo uongozi jumla wa chama wakiwemo katibu mkuu, Andrea Nahles, na makamo wenyeviti, Hannelore Kraft, Aydan Özguz, Olaf Scholz na Manuela Schwesig, watapigania upya nyadhifa zao. Nafasi ya meya wa jiji la Berlin, Klaus Wowereit, aliyeamua kutopigania tena wadhifa wake chamani, itagombewa na mwenyekiti wa chama cha SPD katika jimbo la Hessen, Thorsten Schäfer-Gümbel.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/dpa/AFP
Mhariri: Josephat Charo