Leo ni siku 100 tangu COVID-19 kuthibitishwa Ujerumani
6 Mei 2020Ilikuwa tarehe 27 Januari mwaka huu mgonjwa wa kwanza mwenye maambukizi ya virusi vya corona alipothibitishwa karibu na jiji la Munich kusini mashariki mwa Ujerumani. Mtu huyo tayari amepona, na namna alivyoshughulikiwa imekuwa mfano unaofuatwa kwa watu wengine takribani 160,000 waliopatwa na ugonjwa wa COVID-19 hadi sasa nchini Ujerumani.
Mkakati umekuwa ule ule wa kuwapima watu, kuwatenga wenye maambukizi, na kufuatilia hali ya wale waliokutana na wagonjwa hao. Matokeo ya mkakati huo ni kwamba Ujerumani imefanikiwa kupunguza idadi ya vifo ikilinganishwa na nchi nyingine za Ulaya na Marekani, na mfumo wake wa afya kamwe haujakaribia kulemewa.
Ujerumani yaweza kuepuka shari kamili
Mkuu wa Taasisi ya Robert Koch ambayo inaratibu mapambano dhidi ya virusi vya corona nchini Ujeruani, Lothar Wieler, amesema hivi karibuni kwamba hadi sasa mambo yamekwenda kulingana na matarajio yao.
''Lengo letu ni kuwalinda wakaazi wote wa Ujerumani dhidi ya COVID-19 kwa njia bora inayowezekana. Kwa kulinganisha na nchi nyingine, naweza kusema sisi Ujerumani tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa'', amesema Wieler.
Hali ya maisha imebadilika sana nchini Ujerumani katika kipindi hiki cha siku 100. Akizungumza mwishoni mwa mwezi Januari, waziri wa afya Jens Spahn alisema serikali iko macho na imejiandaa vyema. Mwezi Februari haukuwa na mabadiliko makubwa, kwa sababu wakati huo, hakuna aliyefikiria kuwa masharti ya kutotoka nje yanaweza kutangazwa Ujerumani kama ilivyokuwa wakati huo katika mji wa Wuhan nchini China.
Mwezi Machi waizindua nchi kuhusu ukweli wa mambo
Mambo yaligeuka kabisa katikati ya mwezi Machi, pale Kansela Angela Merkel alipovunja kimya chake na kulihutubia taifa. Katika mkutano na waandishi wa habari Machi 11, Bi Merkel alitahadharisha, kuwa upo uwezekano wa asilimia 60 hadi 70 ya Wajerumani wote kukumbwa na maambukizi ya virusi vya corona.
Hapo ilibidi kuukodolea macho ukweli wa hali halisi, na mnamo Machi 18, Kansela Merkel alitanabahisha kwamba Covid-19 ndicho kitisho kikubwa zaidi kwa Ujerumani tangu kumalizika kwa vita vikuu vya pili vya dunia. Mipaka ya nchi ilifungwa, sambamba na shule na vyuo na shughuli nyingi za kibiashara na maisha ya kawaida. Uongozi wa Kansela Merkel mnamo kipindi cha janga hili umefufua umaarufu wake uliokuwa umeporomoka vibaya.
Zimekuwepo nadharia nyingi kuhusu sababu ya Ujerumani kutokuwa na vifo vingi vya corona, lakini inaaminika kuwa siri ilikuwa kuchukua tahadhari mapema, na kuwapima watu wengi inavyowezekana.
Waziri wa Afya Jens Spahn anasema Ujerumani haina haja ya kuwa na majivuno, na kuhimiza kuwa makini wakati masharti ya karantini yakilegezwa na kujaribu kuyarudisha maisha katika hali yake ya kawaida.