Siku 100 za Nahles kwenye kiti cha SPD
1 Agosti 2018Hakuna shamrashamra nyingi katika maadhimisho ya siku ya Jumatano (Agosti 1) ambapo alitarajiwa kukutana na meya wa mji wa Dietfurt wenye wakaazi 6,100 na kisha kumalizia siku yake kwa kutembelea kiwanda cha utengenezaji pombe katika jimbo hilo.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo wa SPD anabidi kutimiza wajibu wake ikiwa anataka kukabiliana na mtazamo uliyopo sasa kuelekea chama chake, ambacho hakijawahi kuwa na nguvu katika jimbo la Bavaria na hata kura za maoni za karibuni zinaonesha kwamba kimeporomoka hadi asilimia 13 - fedheha nyingine katika historia ya chama hicho.
"Pamoja na yote, hata kwa wale wanaompinga kwenye chama chake cha SPD, Nahles ameonekana kukiunganisha chama" anasema Johannes Kahrs kutoka kundi la wahafidhina linalojulikana kama Seeheimer Kreis ndani ya chama cha SPD.
Mwanasiasa huyo anasema kwamba licha ya kutokuwa mfuasi au shabiki wa Nahles na kundi lake, anakiri kwamba bibi huyo anayaendesha mambo barabara. Kiongozi wa tawi la vijana wa chama cha SPD linalofahamika kama Jusos, Kevin Kühnert, anaunga mkono pia mtazamo huo,akisema: "Bi Nahles anaonesha juhudi za kupindukia. Anatumia muda wake mwingi kufanya mahojiano na kupokea simu mapema kabisa asubuhi au hata usiku."
Matazamio ya Nahles
Mwanamama huyo mwenye umri wa miaka 48 bila shaka angependa kusikia hali mbaya ya chama chake haipo, lakini hilo bado lina mashaka.
Katika uchaguzi wa mwaka jana, matokeo ya uchaguzi mkuu ya asilimia 20.5 yameporomoka na kufikia asilimia 18. Lakini juu ya hilo wanaharakati wengi wa SPD wanahisi ni mapema mno kumhukumu Nahles.
Kwa mfano, miongoni wa wenye mtazamo huo ni kiongozi wa SPD katika jimbo la Oberhausen Mashariki, Maximillian Janetzki mwenye umri wa miaka 28, ambaye pia ameshiriki kuandika tathmini ya chama.
Janetzki aliiambia Deutsche Welle kwamba Nahles anafahamu kwamba huwezi kulinganisha chaguzi moja na nyingine, lakini anabidi atilie maanani kwamba chama cha SPD pia kinabidi kutumia kipindi hiki cha kuwepo serikalini kujiimarisha.
Nahles amelazimika kuibadili lugha ya serikali kuifanya iwe lugha ya chama cha SPD kitu ambacho pia kilipendekezwa katika tahmini ya ndani ya chama chake baada ya matokeo mabaya ya uchaguzi wa mwaka 2017.
Kwa yale anayoyapitia hivi sasa, Nahles amebaini kwamba hakuna kazi rahisi. Kichekesho cha mambo ni kwamba kinachowatia wasiwasi zaidi Wajerumani ni masuala ya kijamii kuliko kitu kingine chochote, masuala ambayo yaliwahi kushughulikiwa na chama cha SPD kwa ufanisi mkubwa - kuanzia suala la umasikini kwa wazee, usawa katika elimu pamoja na gharama nafuu za kodi ya nyumba.
Yote haya Janetzki anataraji kwamba chama kitayakumbuka. "SPD na Andrea Nahles wanapaswa sasa kuona kwamba tumeshaondokana tena na mvurugano wa suala la wakimbizi. Ni lazima lishughulikiwe suala la gharama ya maisha, suala la sekta ya wanaopata mshahara wa chini na pamoja na suala la kukosekana usawa katika masuala ya kijamii nchini Ujerumani."
Mwandishi: Jefferson Chase/Saumu Mwasimba
Mhariri: Iddi Ssessanga