1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku 100 za Rais Tshisekedi madarakani, amefanikisha nini?

Saleh Mwanamilongo, Kinshasa6 Mei 2019

Rais Felix Tshisekedi ameitimiza siku mia moja tangu kuapishwa kwake, lakini hadi leo bado Wakongomani wangali wanasubiri kuona mageuzi aliyoahidi ikiwemo kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi wa serikali.

Präsident des Kongos: Felix Tshisekedi
Picha: Getty Images/S. Maina

Rais Felix Tshisekedi ameitimiza siku mia moja tangu kuapishwa kwake, lakini hadi leo bado Wakongomani wangali wanasubiri kuona mageuzi aliyoahidi ikiwemo kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi wa serikali.  Hadi sasa, bado mkuu huyo wa nchi hajamteuwa waziri mkuu wala kuunda serikali mpya miezi minne baada ya uchaguzi. 

Kwenye hotuba aliyoitoa Rais Felix Tshisekedi kwenye mwanzoni mwa mwezi Machi alipozinduwa mpango wa haraka wa siku mia moja. Rais Tshisekedi alisema "Mnamo siku mia moja za utawala wangu, nitakuwa nimeshakamilisha baadhi ya miradi kwenye sekta ya usalama, siasa, jamii, uchumi, miundombinu na huduma kwa vijana."

Ahadi hizo za Rais Tshisekedi zilitarajiwa kutekelezwa na serikali mpya, lakini hadi sasa bado hajateuwa waziri mkuu ambaye ndiye anapaswa kuunda baraza hilo la mawaziri la serikali mpya.

Mjini Kinshasa, kwa mfano, kunashuhudiwa miradi kadhaa ya utengenezaji wa barabara. Shirika la ujenzi wa barabara lilielezea kwamba mnamo kipindi cha siku mia moja za utawala wa Tshisekedi ingelitengeneza kilomita  40, lakini hadi sasa ni chini ya kilomita 20 zilizotengenezwa.

Upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unaukosoa utawala wa Rais Tshisekedi akiwa ametawala tu kwa siku 100.Picha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Wakati siku hizi mia moja zikitimu, upinzani unaukosoa vikali utawala wa Rais Tshisekedi. Kiongozi wa vuguvugu la Lamuka, Martin Fayulu, amesema kwamba anachofanya Tshisekedi mnamo kipindi hiki ni kuponda fedha za umma kwa safari za kila siku.

Kwa upande wake,Valentin Mubake, mshirika wa zamani wa Etienne Tshisekedi, anasema kutokuwepo kwa serikali mpya kunaonyesha wazi udhaifu wa uongozi wa Felix Tshisekedi:

"Walitafuta madaraka kwa ajili ya madaraka tu. Ni mieizi minne sasa hakuna waziri mkuu, hakuna serikali, na hakuna chochote walichokifanya ama watakachokifanya."

Hata hivyo, Rais Tshisekedi anasifiwa na mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa hatua za mwanzo alizochukuwa, hasa kwa kuwaachia huru wafungwa mia saba wakiwemo wale wa kisiasa. Na vilevile kumruhusu Moise Katumbi kurejea nchini.

Tshisekedi aliahidi pia kurejesha usalama huko mashariki mwa nchi, na vile vile kupambana na rushwa mnamo kipindi cha siku mia moja.

Rais Tshisekedi aliahidi atahakikisha vyombo vya kisheria vinasimamiwa na watu wenye maadiliPicha: picture-alliance/dpa/M. Gambarini

"Kwenye sekta nyingine muhimu ikiwemo ile ya kisheria, nitahakikisha kwamba vyombo vya kisheria vinamilikiwa na watu wenye maadili bora na wasio na utovu wa nidhamu, ambao watapambana na rushwa iliyokithiri nchini."

Lakini, wakati Kongo imeshuhudia kujisalimisha kwa baadhi ya wapiganaji huko Kivu na Kassai, bado kumekuwa na mashambulizi kadhaa dhidi ya jeshi kwenye majimbo Kivu ya Kaskazini na Ituri.

Hapa mjini Kinshasa, watu wana maoni tofauti kuhusu utekelezwaji wa ahadi za Rais Tshisekedi. Wengi wanahisi kwamba hakujakuweko na mabadiliko makubwa, mfano wa Muyaya Luaba, mkaazi wa mkoa wa Lemba, mashariki mwa jiji la Kinshasa:

"Hakuna madaliko hata, hali ni ileile, wewe ni mwadishi habari na unafahamu vyema kwamba hali bado ni mbovu."

Utafiti uliondeshwa na shirika la maoni la TARGET SARL mwezi Machi ulielezea kwamba asilimia 53 ya raia wa Kongo waliridhika na siku 30 ya utawala wa Felix Tshisekedi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW