Siku 100 za serikali ya Ujerumani
21 Juni 2018Tukianza na gazeti la Manheimer Morgen, mhariri anaandika kuhusu siku 100 tangu kuingia madarakani serikali ya muungano nchini Ujerumani. Mhariri anaandika:
"Kansela Angela Merkel na chama chake atapungukiwa na viti viwili tu bungeni iwapo chama ndugu cha CSU kitajitoa katika muungano unaounda serikali. Hatua kama hiyo itakuwa ni mapinduzi makubwa kwa kipindi chote cha bunge kilichobakia.
Kwa kuwa katika wowote ule Ujerumani inapaswa kwa kiasi fulani kupumua baada ya mwaka mmoja wa viongozi kudhoofisha. Kile kinachosababisha wasi wasi, ni kwamba mbali na chama cha Kijani, ambacho wakati ule kilionekana kuwa katika nafasi ya kimkakati, vyama vyote vingine vilikuwa vinajitathmini, kuhusiana na fursa ndogo walizonazo wakati huo ama baadaye."
Mhariri wa Gazeti la Weser-Kurier la mjini Bremen, akiandika kuhusu siku 100 za serikali ya muungano ya Ujerumani anasema, kitisho cha chama cha CSU kujitoa katika ushirika na chama cha kansela Angela Merkel cha CDU hatimaye kimekwisha. Mhariri anaendelea:
"Hali hiyo inavutia kwa kila upande. Lakini chama cha CSU hakitaki kuikumbatia hali hiyo. Chama hicho kinataka kuendelea kufuata mkakati wake, kama ambavyo viongozi wa chama hicho Horst Seehofer na Markus Soeder walivyojipanga. Kitisho cha kuvunja umoja wa vyama hivyo ni makelele ya bure. Kujitoa katika kushiriki katika serikali , kutakuwa na maana tu ya kuweka haki ya kiliberali ya waombaji hifadhi kupitia chama cha Kijani. Kila la kheri katika uchaguzi wa jimbo la Bavaria, na kwa ukweli muda unayoyoma sio kwa Merkel , lakini kwa chama cha CSU. Chama hicho kinapaswa hadi Juni 30 kupata jibu mjarabu, kwanini kiendelee kufuata njia ya kansela, wakati binafsi hakiwezi kupata jibu linalostahili kutoka katika mkutano wa Umoja wa Ulaya."
Kuhusiana na mkutano maalum kati ya kansela Merkel na Umoja wa Ulaya kuhusu sera za kuomba hifadhi katika mataifa ya Umoja huo, mhariri wa gazeti la Neue Osnabrueker Zeitung anaandika.
"Katika Umoja wa Ulaya, anayetaka kuidhinisha kitu , ni lazima kimsingi amsaidie mwingine. Hali hii anaifahamu bila shaka kansela Merkel kuliko mtu mwingine yeyote. Anafahamu kwamba kupata kuungwa mkono na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya katika mzozo wa wahamiaji katika mkutano maalum ni lazima kutoa chochote. Hiyo ni nafasi kwa serikali nyingine za Umoja wa Ulaya, kuweka sawa mambo mengine ya zamani. Bila shaka nchi kama Ugiriki yenye madeni mpaka puani, ambayo mpango wake wa msaada unafikia mwisho mwezi Agosti, itataka kwa njia moja au nyingine Ujerumani itoe msaada. Hii ina maana wakimbizi kwa unafuu wa madeni ? Ama wakimbizi kwa bajeti ya eneo la sarafu ya euro, kama inavyotaka Ufaransa ? Merkel anajitumbukiza katika mkanganyiko mwenyewe, ambao kujitoa itamlazimu kutumia fedha, na itakuwa kuwabebesha mzigo walipa kodi wa Ujerumani."
Gazeti la Frankfurt Rundschau likiandika kuhusu kujitoa kwa Marekani katika baraza la Umoja wa mataifa la haki za binadamu, mhariri anaandika.
"Kujitoa kwa Marekani hakutakuwa na athari zozote, na pia hali ya haki za binadamu haitakuwa bora zaidi. Baraza hilo ni mara chache linapata haraka suluhisho katika suala hilo. Mjadala utakaoendelea kuwapo unachangia katika diplomasia , na mfano ni kuhusu mpango wa kinyuklia wa Iran unaothibitisha kuhusu majadiliano ambayo hayaleti tija."
Ni maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani kama yalivyokusanywa na Sekione Kitojo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga