Siku 100 za Trump: Marekani yakabiliwa na mabadiliko makubwa
29 Aprili 2025
Januari 20, 2025, ndio ulikuwa mwanzo wa urais kwa mara ya pili kwa Donald Trump. Tangu aingie madarakani, mengi yamebadilika katika siasa za Marekani kiasi kwamba ni vigumu kuamini kuwa ni siku 100 tu zilizopita.
Iwe ni mabadiliko ya kimsingi katika sera ya mambo ya nje ya Marekani au kuweka ushuru kwa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje, hakuna hata siku moja inayopita bila Ikulu ya White House kutumika kama chanzo cha "habari muhimu" za dharura.
Utawala huu wa pili wa Trump unaigawanya nchi kuliko hapo awali. Hata wakati hayo yanafanyika, wengi wanauliza: Je, ni ahadi ngapi kati ya ahadi ambazo Trump alitoa kwa wafuasi wake kabla ya uchaguzi wa Novemba mwaka jana, ambazo rais huyo wa Marekani kweli ametimiza?
Kumaliza vita vya Ukraine
Mnamo Mei 2023, katika hafla moja jimboni New Hampshire, Trump alisema ikiwa atachaguliwa, atamaliza vita vya Ukraine mara moja. Alisema na hapa namnukuu, "Wanakufa, Warusi na Waukraine. Ningesitisha vifo hivyo. Ningefanya hivyo katika saa 24.” Alisema. Lakini vita bado vinaendelea, na Trump amelazimika kukiri kwamba hajaweza kumaliza mzozo huo.
Utawala wa Trump unashughulikia aina Fulani ya suluhisho la upande mmoja, lakini bila ya uungaji mkono wa washirika wa jadi wa Marekani na kwa makubaliano yanayoonekana kuwapendelea Warusi kuliko Waukraine. Sio Ukraine tu. Washirika wa magharibi wa Marekani pia wana wasiwasi kuhusu uliko msimamo wake Trump katika mzozo huo.
Trump: kuwatimuwa wahalifu
Sera ya uhamiaji ilikuwa moja ya masuala ya kampeni ya Trump. Kwenye hafla mjini New York Oktoba 2024, aliahidi kuwa kama atachaguliwa, ataanzisha mpango mkubwa kabisa wa kuwafukuza wahamiaji haramukuwahi kushuhudiwa katika historia ya Marekani.
Trump alisema "atawaweka jela wahalifu hawa waovu wanaosababisha umwagaji damu, kisha kuwafukuza katika nchi yetu haraka iwezekanavyo."
Mpaka sasa, mpango huo wa kuwafukuza wahamiaji haramu haujafanyika kwa kasi. Mwezi Februari, ambao ulikuwa wa kwanza kamili tangu kuingia madarakani, serikali ya Marekani iliwafukuza karibu wahamiaji 11,000. Katika kipindi hicho mwaka wa 2021, mwezi wa kwanza wa utawala wa Joe Biden, idadi hiyo ilikuwa karibu 12,000.
Hata hivyo, inaripotiwa kuwa watu wachache wanavuka mpaka wa kusini na Mexico na kuingia Marekani chini ya Trump.
Uchumi: ‘Marekani imerudi'
Trump alifanya kampeni akiahidi kuwa uchumi wa Marekani utaimarika chini ya uongozi wake. Moja ya kaulimbiu zake ilikuwa "kuifanya Marekani kuwa nafuu tena" – bei zitashuka katika siku yake ya kwanza serikalini, aliahidi. Hii imetokea kwa baadhi ya bidhaa, kama vile petroli. Bei za safari za ndege na za vyumba vya hoteli pia zimepungua kama tu ilivyo kwa mfumko wa bei.
Stephen Miran, mwenyekiti wa Baraza la Washauri wa Kiuchumi, katika Ikulu ya White House, alisema katika televisheni ya CNBC kuwa sera za Trump zinafanya kazi katika kuupunguza mfumko wa bei.
Hata hivyo, kwa Wamarekani wengi, manunuzi katika madula ya jumla bado ni ghali kama tu ilivyokuwa wakati Trump alipoingia usukani.
Ushuru wa Trump: Ahadi ilitimizwa, sababu ya kuwa na wasiwasi?
Baada ya kuchaguliwa kwake, Trump alitangaza kwamba atakomesha sera ya "mipaka iliyo wazi kabisa" na nakisi ya kibiashara ya Marekani. Mnamo Aprili, utawala wa Trump ulianzisha mfululizo wa ushuru wa kinga kwa karibu bidhaa zote zinazoingizwa Marekani. Kwa hivyo: ahadi imetimizwa.
Hata hivyo, hii inafanya baadhi ya bidhaa kuwa ghali zaidi kwa watumiaji wa Marekani na kuhujumu mahusiano yaliyopo ya kibiashara. Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew, Wamarekani sasa wanaitazama hali ya uchumi wa nchi yao na mustakabali wake kwa umakini zaidi kuliko walivyofanya mwezi Februari, muda mfupi baada ya Trump kuchukua madaraka, na kabla ya kutangaza ushuru wake.
Makala hii imetafsiriwa kutoka Kijerumani