Siku tano za makabiliano: Israel na Iran zaendelea kufumuana
17 Juni 2025
Israel na Iran zimeendelea kurushiana makombora kwa siku ya tano mfululizo katika kile kinachoelezwa kuwa makabiliano ya moja kwa moja na yenye ukali zaidi kuwahi kushuhudiwa kati ya mahasimu hao wawili.
Kutoka kwa vita vya uwakala na operesheni za siri, hali sasa imebadilika na kuwa vita vya wazi – hali inayozua hofu kubwa ya kuibuka kwa vita vikubwa katika Mashariki ya Kati.
Israel ilitangaza Jumanne kwamba ilifanya mashambulizi makubwa dhidi ya vituo vya droni na makombora magharibi mwa Iran, hasa katika jiji la Tabriz. Milipuko pia ilisikika mjini Tehran na Natanz, maeneo yenye mitambo ya nyuklia. Iran ilijibu kwa mashambulizi mapya ya droni na makombora, huku kamanda wake Kiumars Heydari akisema yataongezwa ukubwa.
Wakati huo huo, Iran imeripoti vifo vya watu wasiopungua 224 na zaidi ya 1,200 kujeruhiwa, huku Israel ikithibitisha vifo vya raia 24 na kuwahamisha zaidi ya watu 3,000. Miji ya Tel Aviv na Jerusalem imeshuhudia tahadhari za mashambulizi huku vipande vya makombora vikisababisha uharibifu.
Malengo ya Israel: Kuzuia Iran kumiliki silaha za nyuklia
Jeshi la Israel linasema limeharibu theluthi moja ya mifumo ya makombora ya Iran na kumuua mkuu wa majeshi wa wakati wa vita. Msemaji wa jeshi Effie Defrin alidai kuwa sasa Israel inadhibiti anga ya Tehran. Hata hivyo, vyombo vya habari vya kimataifa vimeripotiwa kukabiliwa na vikwazo nchini Israel katika kuripoti mashambulizi hayo.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema kampeni ya kijeshi inalenga kusambaratisha mpango wa nyuklia wa Iran, uwezo wake wa kutengeneza makombora, na kuangamiza mitandao ya ugaidi. Alidokeza pia uwezekano wa kulenga viongozi wa ngazi ya juu wa Iran.
Iran, kupitia televisheni yake ya taifa, imeituhumu Israel kwa kuanzisha uhalifu wa kivita na kutangaza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya maeneo nyeti ya kiusalama na makazi ya makamanda wa kijeshi wa Israel.
Tahadhari kutoka kwa Trump na hatua za mataifa mengine
Rais wa Marekani Donald Trump amewataka wakazi wa Tehran kuhama mara moja na kudokeza uwezekano wa kutuma wajumbe kama Makamu wake JD Vance kwa mazungumzo. Lakini pia amesisitiza kuwa kuondoka kwake mapema kwenye mkutano wa G7 hakuhusiani na kutafuta usitishaji wa mapigano, bali mpango mkubwa zaidi.
China, India, Thailand na baadhi ya mataifa ya Ulaya tayari yameanza kuwaondoa raia wao kutoka maeneo ya hatari. Slovakia na Jamhuri ya Czech zimepokea ndege za kuwahamisha wakimbizi wa vita kutoka Israel na Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Guo Jiakun, alisema: "Hali ya Mashariki ya Kati imezidi kuzorota ghafla, hali isiyofaa kwa upande wowote. Kuchochea moto, kutoa vitisho na kuongeza mashinikizo hakutapunguza mvutano bali kutachochea mzozo zaidi."
China imetoa wito kwa pande zote husika, hasa zile zenye ushawishi kwa Israel, kuwajibika na kuchukua hatua za haraka ili kuzuia kuenea kwa mzozo huu.
Mazungumzo ya nyuklia yavurugika, hofu yazidi
Mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na Marekani yamesitishwa kufuatia mashambulizi ya Israel, ingawa Tehran imedokeza kuwa inaweza kuonyesha utayari wa maelewano iwapo kutakuwa na usitishaji wa mashambulizi. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, ameonya kuwa mashambulizi yakiendelea, Iran nayo itajibu kwa nguvu zaidi.
Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) limethibitisha uharibifu mkubwa katika kituo cha nyuklia cha Natanz, ambapo mashine 15,000 za kurutubisha urani zinahofiwa kutofanya kazi.
Viongozi wa dunia, akiwemo Emmanuel Macron na Recep Tayyip Erdoğan, pamoja na kundi la G7, wametoa wito wa kupunguza mvutano na kuizuia Iran kumiliki silaha za nyuklia, wakionya juu ya tishio la vita vikubwa vya kikanda.
Chanzo: Mashirika