Siku ya afya dunian-tarehe 7 Aprilii:
6 Aprili 2006Leo ni siku ya afya duniani na wakati ikiadhimishwa siku hii, kinachojadiliwa nchini Kenya ni suala la huduma duni kwa wafanyakazi wa sekta ya afya nchini humo. Mishahara ya madaktari na wafanyakazi wengine wa sekta ya afya serikalini ni ya chini mno kiasi ya kwamba hawatoi huduma zao kwa muda unaotakiwa kila siku kama wanavyofanya katika hospitali za binafsi . Kwa mfano Mwenyekiti wa chama cha madaktari nchini Kenya Dr Stephen Ochiel anasema fedha anazopata Chuo kikuu hazitoshi hata kukidhi mahitaji yake ya chakula kwa mwezi .
Kwa mujibu wa maafisa wa afya, baadhi katika ngazi ya chini ya taaluma hiyo hulipwa chini ya dola 121 kwa mwezi, wakati wenzao katika sekta ya binafsi hulipwa mara kumi zaidi ya mshahara huo unaolipwa na hospitali za serikali. Lakini pamoja na hayo hali ni mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini. Madaktari katika sehemu hizo hawawezi kufanya kazi katika hospitali za binafsi kwa sababu wengi miongoni mwa wakaazi ni masikini na hawawezi kumudu kulipia gharama za matibabu katika taasisi hizo za binafsi. Matokeo yake kwa hivyo huwa ni upungufu wa wafanyakazi wa huduma ya afya katika maeneo hayo.
Tatizo kama hilo lilionekana mwaka jana baada ya mapigano ya kikabila katika eneo la Turbi kaskazini mwa Kenya. Watu 60 waliuwawa katika mapigano hayo na mamia wengine wakajeruhiwa vibaya na kupelekwa katika hospitali ya wilaya ambayo ilikua na daktari mmoja wa kuwatibu.Mishahara ya chini imewasababisha madaktari na wauguzi yaani manesi kutafuta ajira katika nchi za nje kama Marekani, Canada, Uingereza, Australia na nchi za kusini mwa Afrika, ambako masharti ya kazi na tija ni bora zaidi.
Ingawa hakuna tarakimu rasmi zilizokusanywa kujua idadi kamili ya wafanyakazi wa sekta ya afya walioiahama Kenya kutafuta maisha bora n´gambo, hata hivyo maafisa wanaamini kwamba idadi yao ni kubwa. Maafisa wa serikali akiwemo Naibu waziri wa afya Enoch Kibunguchy wanasema kuna wauguzi 6,000 wasio na ajira na tatizo ni kwamba hawawezi kuajiriwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha. Hata hivyo mapema wiki hii, Rais Mwai Kibaki alitangaza kwamba serikali yake itawaajiri wafanyakazi wapya 3,200 wa huduma za afya ifikapo Juni mwaka huu, kusaidia kupunguza uhaba wa wafanyakazi ulipo hivi sasa. Kwa jumla kunahitajika wafanyakazi 12,000 katika sekta hiyo.
Takwimu za wizara ya afya zinaonyesha kuna daktari mmoja tu na wauguzi 49 kwa kila watu 100,000 nchini Kenya. Idadi hii ni chini ya kiwango kilichopendekezwa na shirika la afya duniani , cha daktari mmoja kwa kila watu 5,000 .Sambamba na hayo kuna matatizo mengine, Hakuna daktari anayetaka kwenda maeneo ya mbali vijijini kwa sababu hakuna cha kumpa motisha. Pia wanalazimika kufanya kazi katika mazingira magumu ikiwa ni pamoja na uhaba wa zana muhimu.
Siku ya afya duniani leo hii inaadhimishwa kwa kauli mbiu “ Kufanyakazi pamoja kwa ajili ya afya.” Kauli mbiu hii imechaguliwa ili kumulika na kutanabahisha juu ya uhaba wa wafanyakazi katika seta ya afya katika nchi mbali mbali duniani, na kutafakari juu ya njia bora zaidi za kuweza kuwafanya madaktari na wauguzi wabakie katika nchi zao badala ya kuzihama kwenda nchi za nje.