Siku ya afya ya kimataifa
7 Aprili 2009Hii leo walimwengu wanaadhimisha siku ya afya ya kimataifa.Mpango wa Marekani wa kupambana na UKIMWI katika nchi 12 za bara la Afrika umesaidia kupunguza kwa zaidi ya asili mia 10 idadi ya watu wanaokufa kwa ukimwi-hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya mradi huo ulioanzishwa mwaka 2003 na rais wa zamani wa Marekani George W. Bush.
Mradi huo wa miaka mitano uliopewa jina PEPFAR,ulioanzishwa mwanzoni kwa kitita cha dala bilioni 15,umesaidia kuokoa maisha ya watu milioni moja kati ya mwaka 2003 na 2007 katika nchi husika,kutokana na kupatiwa madawa ya kudhibiti maradhi na kusaidia kurefusha umri wa mgonjwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchunguzi kama huo kufanywa tangu mradi huo muhimu kabisa kuanzishwa.
"PEPFAR umepunguza vifo kwa karibu asili mia 10 katika nchi hizo ikilinganishwa na nchi nyengine za kiafrika ambazo hazikufaidika na mradi huo" amesema Dr. Eran Bendavid wa chuo kikuu cha Stanford-California kilichosimamia uchunguzi huo.
"Lakini hatukuona mabadiliko ya virusi vya HIV yaliyosababishwa na mradi huo."Ameongeza kusema muasisi wa ripoti hiyo ya kitivo cha afya cha chuo kikuu cha Stanford California.
Dr. Bendavid amesema ameamua kuchunguza mafungamano ya mradi wa PEPFAR ili kuona kama mradi mwengine mkubwa kama huo wa afya kutoka nje ungeweza pia kufanikiwa.
""Ni kitita kikubwa cha fedha kilicholengwa kuokoa maisha ya binaadam-kwa hivyo maendeleo ya maana yanawezekana" amesisitiza Dr. Bendavid.
Kwa mujibu wa wataalam wa kundi lake,mradi wa Marekani wa kupambana na ukimwi katika nchi kumi na mbili za bara la Afrika,umetenga dala 2450 kwa kila mgonjwa aliyetibiwa.
"Utafiti kama huu ni muhimu kwasababu unaonyesha kile kinachoweza kupatikana kutokana na msaada wa maendeleo"-amesema kwa upande wake Dr. Peter Piot,mwenyekiti wa zamani wa Mpango wa Umoja wa Mataifa wa kupambana na virusi vya HIV na UKIMWI (UNAIDS),anaehisi mradi wa PEPFAR umebadilisha mkondo wa maradhi ya ukimwi.
Itafaa kusema hapa kwamba bunge la Marekani limerefusha mradi huo mwaka jana na kuzidisha kiwango cha fedha toka dala bilioni 15 na kufikia dala bilioni 48.
Tarakimu zilizochapishwa mwishoni mwa mwaka jana na shirika la Afya la umoja wa mataifa zinaashiria kuongezeka idadi ya wahanga wa UKIMWI hadi ifikapo mwaka 2012, na kufikia watu milioni mbili na laki nne wakilinganishwa na wahanga milioni mbili na laki mbili mwaka jana,kabla ya kupungua kwa kadiri nusu ifikapo mwaka 2030.
Muandishi :Hamidou Oummilkheir
Mhariri:Abdul Rahman