Siku ya Chakula Duniani yaadhimishwa
16 Oktoba 2014Madhimisho ya siku ya chakula duniani mwaka huu yamejikita chini ya kauli mbiu "Kuulisha Ulimwengu, Kuilea Dunia" ambayo imechaguliwa kwa lengo la kuongeza hamasa kuhusu kuimarisha kilimo cha familia na cha wakulima wadogo wadogo. Maadhimisho ya leo yananuiwa kuuzindua ulimwengu kuhusu jukumu muhimu la kilimo cha familia katika kuangamiza njaa na umaskini, kuhakikisha kuna usalama wa upatikanaji wa chakula na lishe bora, kuboresha kipato, kusimamia vyema raslimali, kuyalinda mazingira na kufanikisha maendeleo endelevu, hususan katika maeneo ya mikoani.
Baraza kuu la Umoja wa Mataifa limeutangaza mwaka huu wa 2014 kuwa mwaka wa Kilimo cha Familia, katika hatua inayotoa ishara nzito kwamba jumuiya ya kimataifa inautambua mchango muhimu wa wakulima katika familia kuhakikisha kuna usalama wa upatikanaji wa chakula duniani.
Akizungumza kuhusu Siku ya Chakula Duniani, Mkurugenzi wa shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, José Graziano da Silva, amesema kwa kukisadia kilimo cha familia tunaweza kuibadili sekta ambayo imehusishwa vibaya na tatizo la njaa.
Mkurugenzi huyo pia amesema, "Mwaka wa kimataifa wa kilimo cha familia unatupa fursa nzuri kuonyesha ulimwengu jinsi sekta ya kilimo inavyoweza kutoa mchango mkubwa zaidi, kutoa lishe bora na mifumo endelevu ya uzalishaji wa chakula."
Da Silva aidha amesema kuwa ulimwengu sasa una fursa ya kuliangamiza baa la njaa wakati huu tulionao.
Ebola kuzidisha makali ya njaa
Maadhimisho ya leo yanafanyika siku moja baada ya onyo kutolewa kwamba huenda kukatokea tatizo kubwa la uhaba wa chakula kama ugonjwa wa Ebola utaendelea kuenea katika miezi ijayo. Umoja wa Mataifa bado haujafanikiwa kuwafikia watu zaidi ya 750,000 wanaohitaji chakula Afrika Magharibi huku bei zikiongeza kwa kasi kubwa na mashamba yakiachwa.
Mtandao unaotoa onyo la mapema kuhusu njaa, FEWS NET, umesema katika ripoti yake ya Oktoba 10 kama visa vya maambukizi ya Ebola vitafikia kati ya 200,000 - 250,000 kufikia katikati ya mwezi Januari mwakani, idadi kubwa ya watu katika nchi tatu zilizoathirika zaidi na Ebola watakabiliwa na uhaba mkubwa au wa wastani wa chakula.
Mashirika ya Umoja wa Mataifa na asasi zisizo za kiserikali zinajizatiti kuongeza juhudi zao kuepusha kuenea kwa njaa. Mkurugenzi wa shirika la chakula duniani, WFP kanda ya Afrika Magharibi, Denise Brown, amesema katika taarifa yake hapo jana na hapa tunanukuu, "Ulimwengu unajipanga na tunahitaji kuvifikia vijiji vidogo katika maeneo ya mikoani. Ishara zinaonyesha hali itakuwa mbaya kabla kugeuka kuwa nzuri, na hili litategemea na sisi." mwisho wa kumunukuu.
Shirika la WFP limesema linataka kuwafikia watu milioni 1.3 wanaohitaji chakula katika maeneo yaliyoathiriwa sana na Ebola nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea.
Mwandishi: Josephat Charo/APE/fao.org
Mhariri:Yusuf Saumu