"Siku ya hasira ", nchini Libya
17 Februari 2011Makundi ya upinzani nchini Libya yametoa wito leo Alhamis wa kufanya maandamano ambayo yamepewa jina la siku ya kuonyesha ghadhabu, ama hasira. Usiku wa jana watu wanne wameuwawa na watu wengine kadha wamejeruhiwa , wakati katika mji wa Beida , mashariki mwa mji wa Benghazi , waandamanaji walipopambana na majeshi ya usalama.
Waandamanaji wakiimba "Khalas", yaani basi inatosha . Makundi kadha nchini Libya yamekuwa yakitoa wito wa kuwa na siku ya kuonyesha ghadhabu, ama hasira, katika tovuti ya facebook na twita , katika mtandao wa internet.
Tovuti za wanaharakati nchini Libya pamoja na makundi ya kutetea haki za binadamu yenye makao yao mjini London wamesema kuwa mapambano na waandamanaji ambao wanaupinga utawala wa kiongozi wa Libya Moamer Ghadafi yamefanyika jana katika mji wa mashariki wa al-Baida. Majeshi ya usalama na wanamgambo wa kamati za kimapinduzi yametumia silaha kulitawanya kundi la vijana waliokuwa wakiandamana katika mji huo na kusababisha watu wanne kuuwawa na wengine kadha kujeruhiwa.
Kiwango cha maandamano ya leo Alhamis kitakuwa mtihani kwa utawala wa kanali Khadafi, mwenye umri wa miaka 64, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1969, lakini ambaye watawala wenzake katika nchi jirani za Misri na Tunisia wameangushwa kutoka madarakani katika maandamano ya umma katika muda wa mwezi mmoja uliopita.
Kundi moja katika tovuti ya facebook linalohimiza "Siku ya hasira" nchini Libya, ambalo lina wanachama karibu 4,400 siku ya Jumatatu limeshuhudia idadi hiyo ikipanda na kufikia 9,600 ilipofika jana Jumatano kufuatia machafuko katika mji wa Benghazi. Gazeti la Quryna limesema kuwa majeshi ya usalama na waandamanaji wamepambana siku ya Jumanne mjini Benghazi, mji uliopo pia upande wa mashariki ya Libya, katika kile ilichokielezwa kuwa ni juhudi za kuchafua maandamano hayo zinazofanywa na baadhi ya watu katika kundi hilo la waandamanaji.
Tuachieni Benghazi, siku ambayo mlikuwa mkiisubiri imefika, wanasema hivyo waandamanaji wanawake usiku wa kuamkia leo Alhamis.
Kiasi cha waandamanaji 2,000 waliandamana katika mji wa bandari wa Benghazi, wanaeleza watu walioshuhudia. Polisi walijaribu, kulitawanya kundi hilo la waandamanaji kwa mabomu ya kutoa machozi na kuwamwagia maji. lakini inaonekana kuwa leo pia watajitokeza watu wengi zaidi kuandamana.
Kwanini mnatukandamiza, tunataka jibu hivi sasa, waandamanaji wanatoa wito. Wanadai haki zaidi za kiraia na wanaandamana dhidi ya rushwa na ufisadi katika utawala uliopo.
Wakivaa vitambaa vya kijani kichwani na wakibeba picha za viongozi wa mapinduzi mikononi mwao waliingia katika eneo la maandamano. Ujumbe wao ukiwa wazi: Shaka yao ni kwamba maandamano yao ya kudai demokrasia hayatamalizika kwa salama.
Mwandishi : Esther Saoub / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman