1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Kimataifa Kupinga Ukatili Dhidi ya Wanawake

25 Novemba 2020

Ulimwengu unaadhimisha Siku ya Kupambana na Ukatili Dhidi ya Wanawake, huku kaulimbiu ya mwaka huu wa 2020 ikiwa inasema ''Ipake Dunia Rangi ya Chungwa: Nisikie Nami Pia. Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Inaanza na Mimi.'' 

Internationaler Tag gegen Gewalt an Frauen
Picha: picture-alliance/NurPhoto/R. Arroyo Fernandez

Katika ujumbe wake kwa siku hii ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ametoa wito kwa jumuia ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti kwani ukatili huo ni changamoto ya haki za binaadamu duniani.

COVID-19 yazidisha ukatili kwa wanawake

Guterres amebainisha kuwa janga la COVID-19 limedhihirisha zaidi suala la ukatili dhidi ya wanawake kama dharura ya ulimwengu inayohitaji hatua za haraka katika ngazi zote, nafasi zote na watu wote.

Amesema kuporomoka kwa uchumi na jamii kuathirika kutokana na janga la virusi vya corona kunawasukuma wanawake katika umasikini na hatari ya unyanyasaji kuongezeka dhidi yao.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio GuterresPicha: UN

''Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni ugonjwa wa kimataifa unaoleta fedheha kubwa katika jamii zote duniani,'' alisisitiza katibu huyo mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Soma zaidi: COVID-19 yaongeza vurugu dhidi ya wakimbizi wanawake

Kama inavyosema kaulimbiu ya mwaka huu ''Ipake Dunia Rangi ya Chungwa: Nisikie Nami Pia. Kupinga Ukatili wa Kijinsia, Inaanza na Mimi,''  jamii inatakiwa kuangazia haki za wanawake na wasichana na kukataa ukatili dhidi yao, kwa kuwezesha, kuzuia, kushughulikia na kukusanya taarifa zote za ukatili. Rangi ya chungwa ni rangi ya mshikamano, hivyo ukatili huo lazima ukomeshwe.

Ama kwa upande wa Ujerumani, imeripotiwa kuwa kila siku nchini humo mwanaume anajaribu kumuua mwenza wake wa sasa au wa zamani. Jaribio moja kati ya matatu yalifanikiwa. Hata hivyo, wanaharakati wanasema washukiwa wengi hawakamatwi.

Wanawake wa Argentina wakiandamana kupinga ukatili dhidi ya wanawakePicha: picture-alliance/AP Photo/V. R. Caivano

Takwimu mpya zinaonesha kuongezeka kwa unyanyasaji wa majumbani dhidi ya wanawake, huku mwaka 2019 ukiwa na idadi kubwa zaidi ya mauaji ya wanawake. Katika Umoja wa Ulaya, Ujerumani ilishika nafasi ya juu kwa mauaji ya wanawake yanayofanywa na wenza wao mwaka 2018, ambapo wanawake 147 waliuawa. Uingereza ilishika nafasi ya pili kwa wanawake 139 kuuawa na Ufaransa ilishika nafasi ya tatu baada ya wanawake 121 kuuawa.

Julia Schäfer, anayeongoza kitengo cha kuzuia uhalifu katika wizara ya mambo ya ndani ya jimbo la Hesse lililo katikati mwa Ujerumani, anasema mauaji ya aina hiyo hayafanyiki ghafla tu. Schäfer anasema mauaji hayo huwa yanafuatiwa na unyanyasaji dhidi ya wanawake uliodumu kwa miaka kadhaa, ambao huanza kwa kutukanwa, kudhalilishwa na kupata shinikizo la kiuchumi.

Kama ilivyo kwa miaka ya nyuma, maadhimishi hayo yanazinduliwa kwa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambayo itahitimishwa Desemba 10, Siku ya Kimataifa ya Haki za Binaadamu.

(UN https://bit.ly/3fvb3hb, UN Women https://bit.ly/3pYZ8gm, DW https://bit.ly/367XzVD)

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW