1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yawakumbuka wahanga wa Mauaji ya Holocaust

27 Januari 2023

Januari 27 ni siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya kuangamiza dhidi ya Wayahudi, Holocaust. Ujerumani ilianza kuadhimisha siku hii 1996.

International Holocaust Remembrance Day | 2023 Gedenkstätte Auschwitz-Birkenau
Picha: Omar Marques/Getty Images

Umoja wa Mataifa: Onyo dhidi ya chuki na ubaguzi wa rangi

Novemba 2005 Umoja wa Mataifa uliitangaza January 27 kuwa siku ya kimataifa ya kuwakumbuka wahanga wa mauaji ya Holocaust. Umoja huo ulitangaza kuwa Holocaust, ambamo theluthi moja ya Wayahudu na idadi isiyojulikana ya watu wa jamii za wachache waliuawa, itatumika kuwakumbusha watu wote wa zama zote juu ya hatari ya chuki, kutovuliana, na ubaguzi.

Katika siku ya kwanza ya kimataifa ya kumbukumbu ya Holocaust Januari 27, 2006, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Kofi Annan, alisema: "Janga la kipekee la Holocaust haliwezi kufutwa. Kumbukumbu yake inapaswa kuwekwa hai kwa aibu na hofu kwa kadiri kumbukumbu ya mwanadamu itadumu.

Kofi Annan alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati lilipopitishwa Azimio la kuanzisha siku ya Kumbukumbu ya Mauaji ya Holocaust, Januari, 27 kila mwaka.Picha: AP

Kwanini Januari 27?

Januari 27, 1945, vikosi vya jeshi la Kisovieti, maarufu kama "Jeshi Jekundu" vilikuwa vimeikomboa kambi ya mateso ya Auschwitz-Birkenau. Askari hao walikutana na manusura wachache, kifusi cha vyumba vya gesi, maiti na majivu ya waliouawa. Katika kambi ya Auschwitz pekee, takribani watu milioni 1.1 waliuawa, wengi wao, karibu asilimia 90 wakiwa Wayahudi - na Auschwitz ilikuwa moja tu ya maeneo mengi ya mateso na mauaji ya watu wengi na Ujerumani iliyokuwa inatawaliwa na Wanazi barani Ulaya.

Soma pia: 'Chuki dhidi ya Wayahudi inaongezeka tena ulimwenguni'

Hadi kufikia mwisho wa Vita Kuu ya Dunia mwaka 1945, zaidi ya Wayahudi milioni sita, mamia kwa maelfu ya watu wa jamii za Sinti, Roma, watu wenye ulemavu, wapinzani wa kisiasa na wengine waliolengwa na na Wanazi waliangamia.

Kofi Annan alisisitiza: "Kukumbuka pia ni ulinzi kwa wakati ujao. Maafa yaliyofikiwa katika kambi za kifo za Wanazi yalianza kwa chuki, ubaguzi na chuki dhidi ya Wayahudi. Kukumbuka vyanzo hivi kunaweza kutukumbusha daima kuwa macho kwa ishara za onyo."

Uzuwiaji wa mauaji ya kimbari huko mbeleni

Tarehe 27 Januari ni jukumu kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kukumbuka wanaume, wanawake na watoto walioteswa na kuuawa. Azimio Nambari 60/7 linakataza ukanaji wowote wa Mauaji ya Holocaust. Linaunga mkono ubunifu wa programu za elimu kukumbuka Holocaust na kuweka mikakati ya kuzuwia mauaji ya watu wengi huko mbeleni.

Geti hili ni sehemu ya historia isiyopendeza ya kambi ya mateso ya Auschwitz.Picha: Omar Marques/Getty Images

Likinukuu Azimio la Kimataifa la Haki za Kibinadamu, azimio hilo linalaani aina zote za "kutovumiliana kwa kidini, uchochezi, unyanyasaji au vurugu dhidi ya watu binafsi au jamii kwa sababu ya asili yao ya kikabila au imani ya kidini" popote ulimwenguni.

Kumbukumbu nchini Israel: Yom HaShoa

Nchini Israeli, siku kuu ya kumbukumbu siyo 27 Januari, bali Yom HaShoa, ambayo kawaida huangukia mwezi Aprili. Kwa dakika mbili, ving'ora vinalia nchini kote: mabasi, magari, kila mtu anasimama. Watu wanakaa kimya, kuwakumbuka wahanga. Neno linalotumika kimataifa Holocaust linatokana na Kigiriki na maana yake ni "kuchomwa kabisa". Nchini Israeli, wanatumia neno Shoa, "janga".

Soma pia: Ujerumani kuharamisha kitendo cha kukana uhalifu wa kivita na mauaji ya halaiki

"Siku ya Kumbukumbu ya Shoa na Ushujaa wa Wayahudi" ilianzishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1951; ilidhibitiwa kwa usahihi zaidi na sheria mwaka wa 1959. Siku hiyo iko katika mwezi wa Nisani katika kalenda ya Kiyahudi. Ina msingi wake katika Machafuko ya Ghetto ya Warsaw mnamo Aprili 1943.

Kulingana na mila ya Kiyahudi, Siku ya Kumbukumbu huanza jioni ya kabla. Wakati wa sherehe za kumbukumbu, mienge sita huwashwa, ikiashiria wahanga wa Kiyahudi milioni sita. Asubuhi, matukio zaidi yanafuata kwenye tovuti ya kumbukumbu ya Yad Vashem.

Kwenye Yom HaShoa, kuna maandano ya jadi ya kumbukumbu nchini Poland kati ya kambi kuu ya Auschwitz na kambi ya maangamizi ya Auschwitz-Birkenau, umbali wa karibu kilomita tatu, ambako watu wengi zaidi waliuawa. Maandamano hayo ya "Wanaoishi" yanahudhuriwa kawaida na maelfu ya vijana wa Kiyahudi.

Siku ya Kumbukumbu ya Holocaust nchini Ujerumani

Baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa ushindi wa Washirika dhidi ya Ujerumani ya Hitler, ilichukua nusu karne nyingine, hadi 1996 ambapo Rais wa Shirikisho wa wakati huo Roman Herzog alitangaza Januari 27 kuwa siku ya kumbukumbu kwa wahanga wa nadharia za Ujamaa wa Kitaifa. Tangu wakati huo, bendera kwenye majengo ya umma nchini Ujerumani zinapeperushwa nusu mlingoti siku hii. Shule nyingi hufundisha mada katika masomo yao.

Spika wa Bunge la Ujerumani, Bundestag, Baerbel Bas akizunguza bungeni katika kumbukumbu ya wahanga wa mauaji ya maangamizi dhidi ya Wayahudu, Holocaust, Januari 27, 2023.Picha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Soma pia: Israel yawakumbuka wahanga wa Holocaust

Tangu 1996, pia kumekuwa na saa ya kumbukumbu ya wahanga wa Wanazi katika bunge la Ujerumani kwenye siku yenyewe ya kumbukumbu au karibu nayo. Wakati katika miaka ya kwanza walikuwa wanasiasa wengi wa Ujerumani waliotoa hotuba za ukumbusho, tangu wakati huo manusura wengi wa Holocaust na wanasiasa kutoka nchi nyingine pia wamezungumza kuhusu uzoefu wao mbele ya wajumbe wa Bundestag: kutoka Israel, Marekani, Poland, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, Jamhuri ya Czech, Hungary, Urusi au Uingereza. Walitoa simulizi zao za kusisimua na kuonya. "Kamwe tena! Kamwe tena!" alipiga kelele rais wa bunge la Israel Mickey Levy mwaka 2022.

Soma pia: Scholz akosolewa kwa jinsi alivyojibu kauli ya Abbas kuhusu Holocaust

Mnamo mwaka wa 2011, Zoni Weisz, kutoka jamii ya wachache wa Sinti na Roma, alizungumza mbele ya Bunge la Ujerumani kwa mara ya kwanza, na mnamo 2017, jamaa wawili wa wahanga wa kinachojulikana kama euthanasia - mauaji yaliyopangwa ya watu wenye magonjwa makubwa au ulemavu - waliongea kwa mara ya kwanza.

Kwa mara ya kwanza, kumbukumbu ya Januari 27 mwaka huu wa 2023itajikita kwa watu ambao waliteswa chini ya Ujamaa wa Kitaifa kwa sababu ya mwelekeo wao wa kijinsia au utambulisho wa kijinsia. Rozette Kats kutoka Uholanzi, mwathirika wa Holocaust ambaye anatetea jamii ya wachache wanaoteswa kwa sababu za mwelelekeo wao wa kingono, atazungumza bungeni.

Makala hii imetafsiriwa kutoka Kijerumani
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW