1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Umaskini Duniani

Helle Jeppesen / Maja Dreyer17 Oktoba 2005

Kila siku watu 30.000 duniani wanakufa kwa sababu hawana chakula cha kutosha. Licha ya idadi hiyo kuzidi kuongezeka katika miaka 15 iliyopita, leo kwenye Siku ya Kimataifa ya Kuondoa Umaskini Duniani kuna matumaini madogo, kwani kwa kuanzia Malengo ya Millenia Shirika la Umoja wa Mataifa limewahi kubadilisha mawazo juu ya tatizo la umaskini.

Kitongoji cha Etipini nchini Afrika Kusini
Kitongoji cha Etipini nchini Afrika KusiniPicha: AP

Mwanauchumi wa Marekani, Jeffrey Sachs, ambaye ni mwenyekiti wa mradi wa Malengo ya Milenia wa Umoja wa Mataifa, ana matumaini makubwa kwamba hali ya dunia itakuwa bora kati karne ya 21. Anaamini kwamba utandawazi utamsababisha kila mmoja kufikiria duniani kote katika uamuzi wake.

Mabadiliko haya hayamaanishi tu kwamba nchi tajiri zinatoa misaada ya maendeleo kwa nchi zinazoendelea bila hisia kuwa nchi hizo zinanunuliwa, bali pia kwamba nchi za Magharibi zina maslahi yao yenyewe, anasema Bwana Jeffrey Sachs: „Tusipotaka kulipa mabilioni machache ya Dola kila mwaka ili kwa mfano kupiga vita Malaria, Ukimwi au kuneemesha hali ya mazingira barani Afrika, basi baadaye tutalazimishwa kulipa mabilioni mengi ya Dola za misaada katika hali ya majanga na vita. Ni kama msemo unavyosema: Kinga ni bora kuliko kutibu.“

Jeffrey Sachs ni mmoja wa watunzi wa malengo ya milenia yaliyoamuliwa na nchi za Umoja wa Mataifa mwaka 2000. Malengo haya manane yanayotarajia kufikiwa mwaka 2015 yanahusu kupunguza umaskini na njaa duniani, elimu ya msingi kwa watoto wote, haki sawa kwa wanawake na wanaume, kupunguza idadi ya watoto na akinamama wanaokufa, kupiga vita ugonjwa kama Malaria na Ukimwi, kuneemesha hali ya mazingira pamoja na hali ya kushirikiana baina ya nchi tajiri na maskini.

Lakini siyo lazima tu nchi tajiri zitimize ahadi zao, bali pia nchi maskini zifanye bidii, anasema Bibi Wahu Kaara kutoka Kenya. Bibi Kaara alianzisha Mtandao wa Kimataifa wa mashirika zaidi ya 15.000 unaoitwa „Global Call to Action against poverty“ maanake: „Wito wa Ulimwengu dhidi ya Umaskini“. Juu ya hayo anaratibu mradi wa Malengo ya Millenia katika halmashauri ya kanisa barani Afrika.

Kwa maoni yake watu wa Afrika pia wanachukua msimamo mkali siku hizi. Anasema: „Waafrika hawataki tena kukubali maisha ya kuzitegemea nchi tajiri, maisha ya umaskini na bila ya usawa. Wito wetu kwa serikali zetu za Afrika una hakika: Hatutaki tena samahani, hatutaki tena umaskini. Lazima malengo ya milenia, yaliyotiwa saini na karibu serikali zote za mataifa ya Kiafrika yapewe kipaumbele. Hatutakubali tena rushwa na uzembe katika utawala wetu.“

Bibi Wahu Kaara pia anasema tangu kuanzisha mtandao kupiga vita umaskini mwezi wa Januari mwaka huu idadi ya watu wanaopinga hali ya kutokuwa na usawa duniani inazidi kuongezeka.

Watu kama Wahu Kaara au Jeffrey Sachs wana hakika kwamba kwa kweli uwezekano wa kupunguza umaskini duniani upo sasa. Malengo ya Milenia siyo shabaha ya mwisho, wengine wanaona malengo haya hayafai kabisa. Hata hivyo hatua ya kwanza kwenye njia ya kupiga umaskini imechukuliwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW