Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani
21 Machi 2017Katika kuiadhimisha siku ya kimataifa ya misitu kila mwaka, nchi mbalimbali duniani zinahamasishwa kuendeleza juhudi za kitaifa na kimataifa ili kuandaa na kushiriki katika shughuli zinazohusika na misitu pamoja na miti, kama vile kampeni ya kupanda miti pamoja na midahalo kuhusu misitu. Siku hii huadhimishwa kwa ajili ya kuwafanya watu waelewe umuhimu wa aina zote za misitu duniani, ikiwemo jukumu lake katika mabadiliko ya tabia nchi.
Uwekezaji na usimamiizi endelevu wa misitu
Kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, kaulimbiu ya mwaka huu ya 'Misitu na Nishati', imechaguliwa kutokana na uwekezaji mkubwa katika uvumbuzi wa teknolojia na katika usimamizi endelevu wa misitu kuwa suala muhimu katika kuongeza nafasi ya misitu kama chanzo kikuu cha nishati mbadala.
Kulingana na suala hilo, uwekezaji sasa unaangaziwa zaidi katika mustakabali endelevu ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu na kukuza uchumi wa kijani. Kwa mujibu wa FAO, kuongezeka kwa kaya na jamii yenye vitalu vya miti pamoja na matumizi ya majiko ya kutumia kuni, kunaweza kuwapatia mamilioni ya watu zaidi katika nchi zinazoendelea urahisi wa kupatikana kwa nishati mbadala ambayo ni nafuu na yenye kuaminika.
Maadhimisho ya mwaka huu
Shirika la FAO litaiadhimisha siku hii katika makao makuu ya shirika hilo mjini Roma, Italia, ambapo mkurugenzi wake mkuu, Jose Graziano da Silva, atafungua maadhimisho hayo. Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika maadhimisho haya ni pamoja na majukumu ya misitu na nishati ya kijani katika utekelezaji wa makubaliano ya Paris ya Nationally Determined Contributions, NDCs, ambayo itatolewa na Rais wa Jamhuri ya Fiji, Jioji Konusi Konrote.
Aidha, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Kuenea kwa Jangwa, UNCCD, Monique Barbut, atatoa mada kuhusu suala la kufungamana kwa misitu na nishati, ambalo ni suala muhimu la maendeleo endelevu pamoja na ushujaa katika maisha ya watu. Eva Müller, Mkurugenzi wa Idara ya Sera za Misitu na Ugavi wa Rasilimali katika shirika la FAO, atazindua chapisho la FAO ambalo linazungumzia kipindi cha mpito cha matumizi ya mkaa: thamani ya mkaa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuimarisha maisha ya watu.
Aidha, Müller atatoa mada kuhusu ajenda inayochukuliwa na FAO katika misitu na nishati ya kijani. Naye Makamu wa Rais wa shirika la Metsa, Rikka Joukio, atatoa mada kuhusu mustakabali wa nishati katika jamii katika kuuvumbua mtazamo huo. Maadhimisho hayo yatahitimishwa kwa hotuba itakayotolewa na Maria Helena Semedo, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Hali ya Hewa na Maliasili wa FAO.
Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012 na siku hiyo ilisherehekewa kwa mara ya kwanza Machi 21, 2013.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/FAO http://bit.ly/2mEim9n, UNECE http://bit.ly/2neaXkI
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman