Kufungua fursa za Kiswahili katika zama za kidijitali
7 Julai 2023![Uganda Internationaler Tag von Kiswahili in Kampala](https://static.dw.com/image/66159226_800.webp)
Katika miaka ya 1950 Umoja wa Mataifa ulianzisha kitengo cha lugha ya Kiswahili cha Redio ya Umoja wa Mataifa, na hii leo Kiswahili ndiyo lugha pekee ya Kiafrika iliyomo katika kurugenzi ya mawasiliano ya kimataifa kwenye Umoja wa Mataifa.
Baraza kuu ya Umoja wa Mataifa, kupitia azimio lake nambari 71/328 la Septemba 11, 2017, kuhusu wingi lugha, lilikaribisha utekelezaji wa siku iliyotengwa makhsusi kwa kila moja ya lugha zake rasmi ili kufahamisha na kujenga uelewa wa historia yao, utamaduni na matumizi, na kumhimiza Katibu Mkuu na taasisi kama vile UNESCO kuzingatia kusogeza mpango huo muhimu kwa lugha nyingine zisizo rasmi zinazozungumzwa kote duniani.
Soma pia: Wadau wahimizwa kukitumia Kiswahili katika tafiti
Kwa maana hiyo, kikao cha 41 cha Baraza Kuu la UNESCO kilipitisha azimio namba 41 C/61 linalotambua nafasi ya lugha ya Kiswahili katika kukuza tofauti za kitamaduni, kujenga uelewa na kukuza mazungumzo kati ya ustaarabu na kubainisha haja ya kukuza wingi lugha kama maadili makuu ya Umoja wa Mataifa na jambo muhimu katika mawasiliano ya usawa kati ya watu, ambayo inakuza umoja katika utofauti na uelewa wa kimataifa, uvumilivu na mazungumzo.
Azimio hilo lilitangaza tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani. Kiswahili ni lugha ya kwanza ya Kiafrika kutambuliwa kwa njia hiyo na Umoja wa Mataifa. Na mwaka huu wa 2023 siku hiyo inaadhimishwa kwa mara ya pili.
Kiswahili na wingi lugha: Mafanikio kwa pamoja
Katika jumui ya Afrika Mashariki, maadhimisho ya siku ya Kiswahili yamefanyika mjini Kampala, Uganda, huku visiwani Zanzibar kukifanyika matukio kadhaa ambayo yamewaleta pamoja magwiji na wataalamu wa lugha hiyo adhim. Sherehe za Kampala ziliandaliwa na Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, KAKAMA, kwa ushirikiano na wizara ya masuala ya Afrika Mashariki ya Uganda.
"Tunacholenga katika maadhimisho haya ni kupanga mikakati ya kisera, ya kiutendaji inayoweza kutuelekeza namna tunavyoweza kutumia lugha ya Kiswahili pamoja na lugha nyengine bila kuwa na changamoto," alisema Dk. Caroline Assimwe, naibu Katibu Mtendaji wa KAKAMA.
Soma pia: Uganda:Kiswahili lazima shule za msingi na sekondari
Wajumbe kutoka kila nchi wanachama wameelezea hali ilivyo kuhusiana na mikakati ya ufundishaji na matumizi ya Kiswahili katika mataifa yao. Wametoa mapendekezo kuhusu vipi lugha hiyo ishughulikiwe kwa mikabala anuwai ili raia kutoka zaidi ya makabila 300 kanda hiyo waitumie zaidi katika kufanikisha ushirikiano wa kijamii, kiuchumi na kisiasa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa kauli mbiu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kuadhimisha siku hiyo, mijadala imelenga kuona jinsi Kiswahili chaweza kukuzwa katika mazingira ya wingi-Lugha, lakini kisionekane kuwa chanzo cha lugha za kikabila kupuuzwa. Baadhi ya wasomi wametoa kauli hizi kuhusiana na hilo.
"Ukitaka kutaja jambo la undani kabisa kwa mtu, njia moja ni kutumia lugha ya nyumnbani na lugha hiyo ni Kiswahili na Kiswahili ni lugha ya nyumbani afrika mashariki na kwa hivyo tuwahamasishe wenzetu wanaopendelea sana kuwasiliana kwa Kiingereza," alisema Profesa Kigongo Bukenya, mtaalamu wa Kiswahili kutoka Uganda.
Rais Mwinyi azihimiza balozi za Tanzania kuchangamkia fursa
Akihutubia kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika kilele cha sherehe zilizofanyika visiwani Zanzibar, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi amezihimiza balozi za Tanzania nchi za nje ambazo bado hazijaanzisha madarasa maalum ya kufundisha Kiswahili na kushajiisha utumiaji wa lugha hiyo kwa usahihi.
Rais Mwinyi amesema baadhi ya balozi tayari zimeazisha madarasa hayo na kutaka jitihada zaidi zifanyike kueneza Kiswahili.
Waziri wa Utamduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania Balozi Pindi Chana alisema historia inaonesha lugha ya Kiswahili imetumika katika ukombozi hivyo ni fahari kwa Tanzania kupewa hadhi ya kuwa na kituo cha urithi wa ukombozi wa Afrika.
Pamoja na hilo Kiswahili kinaimarisha mashirikiano ya uchumi, umoja na mahusiano ya kidiplomasia huku matumizi ya lugha ya Kiswahili yakiendelea kushika kazi katika ngazi zote za serikali ikiwemo nyaraka mbali mbali pamoja na mihimili ya serikali kutumia lugha ya kiswahili.
Maadhimisho ya siku ya Kiswahili duniani yalianza Julai mosi kwa matembezi, kufanyika kwa midahalo Zanzibar na Tanzania bara, huku mataifa mengine katika Afrika pia zikihamasika kuadhimisha siku hii (Julai 7) iliyorasimishwa na Umoja wa Mataifa mwaka jana.
Lubega Emmanuel na Salma Said wamechangia ripoti hii.