1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUlaya

Mazungumzo ya Urusi na Ukraine: Matumaini hafifu

Bakari Ubena (dpa, ap, reuters, afp)
18 Februari 2026

Wajumbe wa Urusi na Ukraine wamekutana Jumanne mjini Geneva kwenye duru nyingine ya mazungumzo ya kuvimaliza vita vya Ukraine, chini ya usimamizi wa Marekani. Lakini matumaini ya kufikiwa makubaliano ni hafifu.

Geneva I Mazungumzo ya amani kati ya Urusi na Ukraine yakisimamiwa na Marekani
Chini ya usimamizi wa Marekani, Wajumbe wa Urusi na Ukraine wakikutana mjini Geneva nchini Uswisi kwenye duru nyingine ya mazungumzo ya kuvimaliza vita vya Ukraine.Picha: Ekaterina Chesnokova/SNA/IMAGO

Wapatanishi wa Ukraine na Urusi wamehitimisha Jumanne  mjini Geneva, siku ya kwanza ya mazungumzo ya amani yanayosimamiwa na Marekani huku kukiwa hakuna dalili zozote zinazoashiria kwamba wamefikia hatua kuelekea kuumaliza mzozo mbaya zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Pili vya Dunia.

Katika mazungumzo hayo, Ikulu ya Kremlin iliwakilishwa na waziri wa zamani wa utamaduni Vladimir Medinsky huku Katibu wa usalama wa taifa wa Ukraine Rustem Umerov akiongoza ujumbe wa Kyiv. Taarifa zinaeleza kuwa matumaini ya kufikiwa makubaliano ni hafifu.

Siku ya pili na ya mwisho katika duru hii ya mazungumzo itafanyika siku ya Jumatano. Marekani imekuwa ikishinikiza kukomeshwa kwa vita hivi vilivyodumu kwa takriban miaka minne, lakini hadi sasa imeshindwa kufanikisha makubaliano kati ya Moscow na Kyiv hasa kuhusu suala muhimu la maeneo ambalo ndilo limekuwa kiini cha tatizo.

Duru mbili za awali za mazungumzo kati ya  Urusi na Ukraine  huko Abu Dhabi hazikuzaa matunda yoyote, huku chanzo kimoja kilicho karibu na ujumbe wa Urusi kilieleza kwa sharti la kutotajwa jina kuwa mazungumzo ya hivi karibuni "yalikuwa magumu mno na yalidumu kwa saa sita."

Zelensky ahoji nia ya Urusi na akosoa shinikizo la Marekani

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akilihutubia taifa kupitia televisheniPicha: Ukrainian Presidential Office/AFP

Katika hotuba yake ya Jumanne usiku, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amesema yuko tayari "kuchukua hatua za haraka kuelekea makubaliano sahihi ya kukomesha vita", lakini akahoji ikiwa Urusi ina nia thabiti ya kufikia makubaliano ya amani kwa kuwa imekuwa ikitoa kipaumbele kwa mashambulizi ya makombora kuliko mchakato wa kidiplomasia.

Hata kabla ya mazungumzo hayo kuanza, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiha ameishutumu Urusi kwa kudhoofisha juhudi za amani baada ya kufanya mashambulizi kwa kufyetua makombora 29 na droni 396 ambayo mamlaka za Ukraine zimesema yalisababisha vifo vya watu wasiopungua wanne na kuwajeruhi wengine kadhaa.  Moscow pia imeilaumu Ukraine kwa kufanya shambulio la droni zaidi ya 150.

Mapema wiki hii, Rais wa Marekani Donald Trump alizidisha shinikizo kwa Ukraine kuitaka kufikia makubaliano haraka na Urusi ambayo inadhibiti karibu theluthi moja ya ardhi ya Ukraine ikiwemo rasi ya Crimea, ambayo ilinyakuliwa kinyume cha sheria mnamo mwaka 2014.

Hata hivyo Zelensky ambaye amesema jana usiku kuwa Trump amekuwa akimshinikiza kuafiki masharti ya makubaliano hayo amesisitiza kuwa nchi yake inatupilia mbali wazo la kuyaachia maeneo ya Donbas ambayo hayajadhibitiwa na Urusi huku akikosoa shinikizo la kujaribu kufikia makubaliano yasiyo na uwiano wala uadilifu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW