1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siku ya mwisho kwa Merkel kupata muafaka wa serikali mseto

Daniel Gakuba
11 Januari 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anayo matumaini ya kupata muafaka hii leo, katika mazungumzo ya matayarisho ya kuunda serikali ya mseto kati ya vyama ndugu vya kihafidhina, CDU/CSU na chama cha Social Democrats, SPD.

Merkel, Seehofer, Schulz
Kuanzia kushoto ni Angela Merkel wa CDU, Horst Seehofer wa CSU na Martin Schulz wa SPD.

Mazungumzo ya leo Alhamis yanatarajiwa kuendelea hadi usiku, kwa sababu viongozi wa vyama vinavyojadiliana, Christian Democratic Union, CDU cha Kansela Angela Merkel na chama ndugu cha jimboni Bavaria cha Christian Social Union CSU, pamoja na chama cha Social Democrats, SPD, asubuhi ya kesho Ijumaa wataripoti kwa maafisa waandamizi wa vyama vyao kuhusu matokeo ya juhudi za siku tano katika kukubaliana kimsingi kuunda serikali ya mseto.

Katibu Mkuu wa CSU Andreas Scheuer amesema mazungumzo hayo ambayo yameendeshwa kwa faragha kubwa yameweka msingi mwema wa kuaminiana. Ingawa vyombo vya habari vimetengwa kabisa katika mchakato wa majadiliano hayo, dalili zimejitokeza kuashiria kwamba mazungumzo hayo ya karibu wiki nzima yameanza kuzaa matunda, yakiwemo kukubaliana juu ya masuala magumu ya sera kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, na sheria ya uhamiaji.

Tetesi za hatua mbele

Vyombo vya habari vimewekewa ngumu katika mazungumzo hayoPicha: picture alliance/dpa/K. Nietfeld

Hali kadhalika, tetesi zimeibuka katika vyombo vya habari kuhusu wanaopigiwa upatu kuongoza wizara muhimu katika serikali mpya ya mseto itakayoongozwa na Kansela Merkel.

Lakini bado Bi Merkel anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuondoa tofauti ndani ya chama chake mwenyewe katika masuala ya kodi kwa matajiri, bima ya afya na utaratibu wa kuzileta nchini Ujerumani familia za wakimbizi waliopewa hifadhi. Kabla ya kuzisawazisha tofauti hizo, uwezekano wake kuongoza muhula wa nne utakuwa bado unakabiliwa na kikwazo. Mkuu wa utumishi katika ofise ya Kansela Angela Merkel, Peter Altmeier, amekiri kwamba bado wana kazi pevu ya kufanya.

''Sote tumeamka mapema kwa sababu bado kuna kazi ngumu inayobaki kufanywa, na tutafanya hivyo faraghani - ambavyo ni sawa. Naamini changamoto zilizopo zitapatiwa ufumbuzi, lakini bado ipo kazi ngumu leo na kesho.'' Amesema Altmeier.

Uamuzi mgumu kwa SPD

Kwa miaka 8 iliyopita, kati ya 12 ya ukansela wa Bi Merkel, chama cha SPD kimekuwa mshirika mdogo katika serikali ya mseto, lakini hivi sasa kinasitasita kuingia tena katika ushirika huo baada ya matokeo mabaya kabisa katika uchaguzi wa Septemba iliyopita.

Chama cha SPD kimepata matokeo mabaya kabisa katika uchaguzi wa Septemba iliyopitaPicha: picture-alliance/dpa/K.Nietfeld

Hata ikiwa ujumbe wa chama hicho chini ya mwenyekiti wake Martin Schulz utafikia makubaliano na Bi Merkel, mazungumzo yoyote rasmi ya kuunda serikali ya pamoja yataidhinishwa katika mkutano wa chama hicho utakaofanyika tarehe 21 mwezi huu wa Januari.

Kwa pamoja vyama vya CDU/CSU na SPD vilipoteza asilimia 13.8 ya wapiga kura ambao katika uchaguzi uliopita walikiunga mkono chama cha Mbadala kwa Ujerumani AfD chenye sera kali za mrengo wa kulia.

Bi Merkel alizidi kudhoofika kisiasa baada ya kushindwa kuunda serikali na vyama vidogo viwili, cha walinzi wa mazingira, the Green, na kinchopendelea biashara, FDP.

Ikitokea mkutano mkuu wa SPD ukapinga kujiunga tena na vyama ndugu vya kihafidhina kuunda serikali, Bi Merkel atalazimika ama kuunda serikali ya walio wachache bungeni, au kuitishwa uchaguzi mpya, hatua ambayo itazidi kuuweka uongozi wake mashakani.

Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, afpe, rtre

Mhariri: Caro Robi

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW